Wanasoka waliowahi kurushiwa ndizi wakiwa uwanjani

Mbrazilii, Dani Alves akila ndizi aliyorushiwa na mashabiki ishara ya ubaguzi wa rangi. Picha na Maktaba
Muktasari:
Kauli ya Blissett imekuja siku chache akiunga mkono uamuzi wa Mbrazili, Dani Alves kuila ndizi aliyorushiwa uwanjani na shabiki mmoja katika mechi ya La Liga kati ya Villarreal na Barcelona Jumapili iliyopita.
MTU mweusi aliyekuwa staa wa Watford enzi hizo, Luther Blissett, aliwahi kusema hivi: “Sikuwahi kununua matunda kwa sababu walikuwa wanikitupia ndizi nyingi sana.”
Kauli ya Blissett imekuja siku chache akiunga mkono uamuzi wa Mbrazili, Dani Alves kuila ndizi aliyorushiwa uwanjani na shabiki mmoja katika mechi ya La Liga kati ya Villarreal na Barcelona Jumapili iliyopita.
Luther Blissett aliungana na wanasoka wengine mastaa kusapoti vita ya kupinga ubaguzi kwenye soka hasa baada ya tukio la Alves kurushiwa ndizi na shabiki.
Staa huyo wa zamani wa England na Watford alikumbana sana na matukio kama hayo ya kurushiwa ndizi na mara kadhaa alijikuta akiwa mpweke kwa kubaguliwa katika miaka ya 1970 na 80.
Mastaa kadhaa akiwamo Mario Balotelli, Bacary Sagna na Sergio Aguero walimsapoti Alves kwa kupiga picha zinazowaonyesha wakila ndizi na kisha wakazituma kwenye mitandao ya kijamii, kitu ambacho kilimkosha sana Blissett, 56, ambaye alibaguliwa sana kutokana na rangi ya ngozi yake enzi hizo.
Wengine waliomsapoti Alves ni nyota wenzake wa Brazil, Oscar, Philippe Coutinho, David Luiz, Neymar, Roberto Carlos, Gilberto Silva na Willian na staa wa Amerika Kusini na Uruguay, Luis Suarez na walimenya ndizi na kuzila kuonyesha kwamba ubaguzi siyo kitu kizuri.
Wakati Villarreal ikibainisha kwamba imemfungia maisha yake yote shabiki aliyemrushia ndizi Alves, beki huyo wa Barcelona, alisema kwamba kama angekuwa na nguvu ya kuipata picha ya shabiki huyo na kuiweka kwenye mtandao wa kijamii ili kila mtu amwone angefanya hivyo.
Hata hivyo, siyo Alves na Blissett pekee waliokumbana na ubaguzi kama huo wa kurushiwa ndizi uwanjani na mashabiki kwa maana ya kuwabagua kwa rangi za ngozi zao na kuwadhihaki kwamba ni wao siyo wanadamu bali ni nyani.
John Barnes
Mmoja kati ya mastaa wa muda wote Liverpool. Katika siku zake za mwanzo za maisha yake ya soka Liverpool, Barnes alikumbana na matukio mengi ya ubaguzi wa rangi kutoka kwa mashabiki wa timu pinzani hadi mashabiki wa timu yake.
Aliwahi kurushiwa ndizi katika pambano la watani wa jadi dhidi ya Everton na picha hiyo imekuwa maarufu mpaka leo ikimuonyesha Barnes akipiga kisigino ndizi hiyo katika Uwanja wa Everton wa Goodison Park.
Barnes pia aliwahi kudai kuwa mashabiki wa Liverpool walimwandikia barua wakimwomba kutojiunga na timu yao. Barnes anadai kwamba aliwahi kusikia wachezaji wa timu yake wakiwabagua wachezaji weusi wa timu pinzani.
Katika tukio moja la kushangaza katika siku zake za awali za maisha ya soka Liverpool, Barnes anadai kwamba dada mmoja aliyekuwa anawaandalia chai wachezaji aliandaa kwa wachezaji wote, lakini kwa kukusudia au kutokusudia hakumwandalia Barnes. Baadaye Barnes alimhoji huku akitania kwa kumuuliza “Ni kwa sababu mimi ni mweusi?’
Neymar
Mwanasoka bora zaidi kwa sasa katika kizazi cha wanasoka wa Brazil, Neymar Da Silva. Huyu naye amewahi kukumbana na mkasa wa kurushiwa ndizi wakati wa pambano la kirafiki kati ya Brazil dhidi ya Scotland Machi 2011 katika Uwanja wa Arsenal, Emirates.
Kinda mmoja Mjerumani ndiye aliyetupa ndizi hiyo uwanjani akimlenga Neymar.
Awali ilidhaniwa kuwa kundi la Wascotland wenye msimamo mkali maarufu kama Tartan Army walikuwa wamefanya tukio hilo, lakini ilipobainika kuwa aliyetupa ndizi alikuwa mtoto wa Kijerumani Chama cha Soka Scotland kilitaka kuombwa msamaha kwa kusingiziwa tukio hilo.
Gael Clichy
Katika hali isiyo ya kawaida katika soka la England, beki wa kushoto wa Manchester City, Gael Clichy alidai kwamba alitupiwa ndizi katika pambano la kirafiki dhidi ya timu ndogo ya Limerick Uwanja wa Thomond Park Agosti 2012 nchini Ireland.
Nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa aliandika katika mtandao wake wa jamii akisema: “Ndizi zimerushwa uwanjani leo wakati watu wakijua kuwa duniani kuna watu wanahitaji chakula.”
Baadaye klabu hiyo ilitoa taarifa kwa kusema: “Limerick FC na Thomond Park watarudi kutazama picha za CCTV na kumjua aliyerusha ndizi hizo uwanjani. Mtu huyo atafungiwa kuhudhuria mechi zozote katika Viwanja vya Thomond Park na Jackman na jambo hilo litapelekwa polisi.”
Mark Walters
Wakati Mark Walters alipojiunga na Rangers ya Scotland kutoka Aston Villa mwaka 1987, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza mweusi kukipiga Rangers.
Pambano lake la kwanza lilikuja Januari 2, 1988 dhidi ya watani wao wa jadi, Celtic katika dimba lililofurika la Parkhead, Scotland. Mashabiki wa Celtic walimpokea kwa kumrushia ndizi na kumpigia kelele za nyani huku wengine wakivaa mavazi ambayo yaliwafanya waonekane kama nyani. Aibu iliyoje!
Roberto Carlos
Huku ikionekana kuwa angemaliza maisha yake ya soka nyumbani kwao Brazil, ghafla Roberto Carlos alipata ofa ya kuichezea klabu ya Anzhi Makhachkala ya Russia. Ni huko ndiko alipokumbana na tukio la ubaguzi wa rangi wakati timu yake ilipokipiga na Krylya Sovetov ya Russia Juni 2011.
Carlos alikaririwa akidai kwamba alifikiria kuachana na soka wakati alipotoka nje ya uwanja kufuatia tukio hilo. “Unajua huzuni inapokukuta. Unapojisikia hauna nguvu ya kufanya lolote. Watoto wengi walikuwepo uwanjani. Jambo hilo inabidi likomeshwe. Nilipokwenda katika vyumba vya kubadilishia nguo wachezaji wenzangu walinikumbatia na kuniimbia nyimbo. Lilikuwa jambo la kuvutia sana. Wachezaji wenzangu wananipenda sana.”
Peter Odemwingie
Tukio jingine la ubaguzi wa rangi nchini Russia. Mwaka 2010 klabu ya Lokomotiv Moscow iliamua kumuuza mshambuliaji wake Peter Odemwingie kwenda klabu ya West Brom ya England. Kuonyesha kwamba mashabiki wa Lokomotiv walikuwa wamefurahi kuondokana na mchezaji mweusi, mashabiki hao walibeba bango lenye picha ya ndizi huku wakiandika ‘Asanteni West Brom’.
Umoja wa soka wa Russia uliitisha kikao cha nidhamu lakini ukaachana na mpango wa kuiadhibu timu hiyo na bosi wa umoja huo alikaririwa akidai kwamba bango la ndizi halikuwa la ubaguzi.
Dan Alves mwenyewe
Hili ni tukio la karibu zaidi na la kusikitisha katika soka. Lilitokea Jumapili iliyopita katika pambano kati ya Villarreal na Barcelona. Wakati Alves akikaribia kupiga kona alirushiwa ndizi ambayo ilitua karibu yake. Aliinama na kuamua kula ndizi hiyo huku akiendelea na mipango yake mingine uwanjani.
Baadaye alisikika akisema: “Tumeumizwa na hilo kwa muda mrefu Hispania. Inabidi ukubali tu tena kwa upole. Hatuwezi kubadili mambo haya kwa urahisi. Kama hautoi umuhimu kwa jambo hilo malengo yao yanakuwa hayatimii.”