Yanga Africa : Kasi mpya,nguvu mpya

Kuanzishwa: Mwaka 1935,
Mahali:Dar es Salaam,
Ubingwa:Mara 24,
Kocha:Ernest Brandts,
Nahodha:Nadir Haroub,
Jezi: Kijani/njano.
Muktasari:
- Timu hiyo iliyoanzishwa mwaka 1935, imechukua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara 24 na kocha wake mkuu wa sasa Mholanzi, Ernest Brandts, anasema wanaanza tena mbio za kuchukua ubingwa mwingine wa 25 msimu huu.
YANGA haikutaka kubadili kikosi chake kilichotwaa ubingwa msimu uliopita. Imeongeza sura chache sana tofauti na mashabiki walivyotarajia kwamba wangesikia majina makubwa yanatua Jangwani kwa nguvu za jeuri ya wanachama matajiri waliopo kwenye kamati ya usajili.
Ingawa habari za uhakika za ndani zinasema kwamba safari hii hakukuwa na bajeti ya kueleweka ya usajili, viongozi na benchi la ufundi wanasisitiza hawakuona haja ya kufanya mabadiliko makubwa kwani timu hiyo inafaa hata kwa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.
Mechi za kirafiki walizocheza zimetoa taswira kuwa bado Yanga itatisha kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara inayoanza leo Jumamosi, Yanga inaanza msimu kwa kucheza na Ashanti jijini Dar es Salaam.
Achana na mechi za kirafiki tu kwani hata Ngao ya Jamii waliyoitwaa wiki iliyopita baada ya kuifunga Azam bao 1-0 Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imezidi kuwaongezea morali ya kufanya vizuri zaidi kwenye ligi.
Ushindani umeongezeka katika kikosi hicho na hiyo inatoa picha kuwa timu itakuwa moto wa kuotea mbali msimu huu wa Ligi Kuu. Timu hiyo iliyoanzishwa mwaka 1935, imechukua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara 24 na kocha wake mkuu wa sasa Mholanzi, Ernest Brandts, anasema wanaanza tena mbio za kuchukua ubingwa mwingine wa 25 msimu huu.
Yanga inafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari ya Loyola iliyopo Mabibo, Dar es Salaam na wakati mwingine kwenye Uwanja wa Bora Kijitonyama, lakini ikitumia Uwanja wa Taifa kama uwanja wake wa nyumbani kwenye mechi za Ligi Kuu.
Timu hiyo inatumia jezi za rangi ya kijani kwenye mechi za nyumbani na njano inapokuwa ugenini huku ikiongozwa na nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na msaidizi wake ni Haruna Niyonzima ‘Fabregas’.
Mikakati yao kwenye ligi
Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Brandts anasema wamejipanga vizuri kukabiliana na ushindani wa timu nyingine zinazoshiriki Ligi Kuu na hawatamdharau yeyote licha ya kikosi chake kuwa bora.
“Tumefanya mazoezi na timu yangu ipo vizuri tayari kwa ligi na tutahakikisha tunacheza kwa uangalifu kwani timu nyingi zimekuwa zikitukamia tunapokutana nazo kwa sababu Yanga ni timu kubwa.
“Nafurahia ubora wa kikosi changu kwani kila nafasi ina wachezaji wengi wazuri na hiyo itatusaidia kama timu kuwa katika kiwango chake kwa muda mrefu na kufanya vizuri kwenye ligi,” anasema Brandts.
“Hofu yangu kubwa ni katika safu ya ushambuliaji ambayo imekuwa ikiniangusha, lakini naamini msimu utakapoanza watabadilika na kufanya kazi, na kama unavyoona katika nafasi hiyo kuna watu wengi hivyo inabidi wajitoe kwa ajili ya timu.
“Siwezi kuwapangia idadi ya mabao ya kufunga kwani kila mmoja anajua majukumu yake ingawa lazima watambue hiyo ni kazi yao lazima waifanye kwa ukamilifu. Kwangu kitu muhimu ni ushindi wa timu hata kama tumefunga bao moja liwe limefungwa na beki, kiungo au mshambuliaji, muhimu nimepata pointi tatu.”
Yanga inanolewa na Brandts anayesaidiwa na Fred Felix Minziro, kocha wa makipa ni Razack Siwa, daktari ni Nassor Matuzya na meneja wa timu ni Hafidh Saleh.
Timu hiyo imesajili wachezaji 29 kwa ajili ya Ligi Kuu Bara ambao ni Ally Mustapha ‘Barthez’, Deogratius Munishi ‘Dida’, Yusuph Abdul, Kelvin Yondani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mbuyu Twite, David Luhende, Juma Abdul, Oscar Joshua, Ibrahim Job, Rajabu Zahir, Haruna Niyonzima ‘Fabregas’, Salum Telela na Athuman Iddi ‘Chuji’.
Wengine ni Frank Domayo, Hamis Thabit, Mrisho Ngassa, Nizar Khalfan, Simon Msuva, Reliant Lusajo, Didier Kavumbagu, Hamis Kiiza, Jerry Tegete, Said Bahanuzi, Hussein Javu, Shaaban Kondo, Issa Ngao, Bakari Masoud na Abdallah Mguhi.