Yanga, Costal Union zashindwa kuonyeshana ubabe

Mashabiki wa timu ya Yanga wakijitahidi kwa udi na uvumba kuishangilia timu yao uwanjani. Picha na Mpigapicha Wetu
Muktasari:
Yanga ilikuwa kambini Antalya, Uturuki na Coastal Union ilikuwa Oman na zote zilicheza mechi kadhaa na timu za huko na kuahidi kwamba zikianza mzunguko wa pili patachimbika.
VUMBI la Kiarabu limetimka mjini Tanga baada ya timu mbili ambazo ni Yanga na Coastal Union zilizokuwa zimepiga kambi kwenye nchi za Kiarabu kushindwa kuonyeshana ubabe.
Yanga ilikuwa kambini Antalya, Uturuki na Coastal Union ilikuwa Oman na zote zilicheza mechi kadhaa na timu za huko na kuahidi kwamba zikianza mzunguko wa pili patachimbika.
Timu hizo zilitoka suluhu jana Jumatano kwenye mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
Matokeo hayo yameishusha Yanga hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu baada ya Azam kuifunga Rhino Rangers bao 1-0 na kufikisha pointi 33 na Yanga ikiwa na 32 sawa na Mbeya City.
Yanga kwenye mchezo huo ilikuwa na kikosi chake kamili huku langoni akisimama kipa Deo Munishi ‘Dida’ na mbele ikiwatumia Didier Kavumbagu na Mrisho Ngassa.
Mchezo ulikuwa na utamu wa aina yake haswa kipindi cha kwanza, timu zilishambuliana na kuonyeshana ufundi huku mwamuzi Simon Mbelwa wa Pwani akizomewa mara kadhaa na mashabiki wa Yanga kwa madai kwamba ameshindwa kuumudu mchezo.
Mashabiki wa Yanga walipigwa butwaa dakika 21 baada ya faulo iliyopigwa kiufundi na kiungo Haruna Niyonzima kupanguliwa na kipa Shaaban Kado ambaye aliwahi kuichezea Yanga.
Abdi Banda aliiandama Yanga mara kadhaa kwenye kipindi cha kwanza lakini alikosa mbinu za kumfunga Dida hata Mkenya, Crispian Odulla dakika 37 alipangua mabeki wote wa Yanga na kupaisha akiwa uso kwa uso na kipa.
Msuva ambaye spidi yake ilionekana kuwachachafya Coastal dakika 41 aliingia kwenye boksi la wapinzani wao lakini akajikuta akianguka mwenyewe baada ya kujigonga.
Ingawa kocha wa Yanga, Hans Pluijm alionekana kukuna kichwa kipindi cha pili, dakika 65 nusura vijana wake wajifunge baada ya Cannavaro kujichanganya alipokuwa akiokoa shuti la Banda lakini mpira ukatoka nje na ikapigwa kona ambayo haikuwa na faida kwa wenyeji.
Wachezaji wapya wa Coastal Haruna Moshi ‘Boban’ na Juma Nyoso walionyesha ukomavu na utulivu wa aina yake uwanjani muda wote, Boban alipiga shuti moja kali kipindi cha pili likagonga besela na kurudi uwanjani Yanga wakaosha.
Mwamuzi wa akiba alionyesha muda wa ziada wa dakika 9 lakini mwamuzi wa kati akachezesha dakika 3 jambo ambalo lililalamikiwa na mashabiki na makocha.
Vikosi vilivyocheza jana; Yanga; Deogratias Munish “Dida”, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub “Cannavaro”, Kelvin Yondani “Cotton”, Frank Domayo, Saimon Msuva, Haruna Niyonzima, Didier Kavumbagu, Mrisho Ngasa/Nizar Khalfan, David Luhende/Jerry Tegete
Coastal; Shaaban Kado, Hamad Juma, Abdi Banda, Juma Nyosso, Mbwana Kibacha, Jerry Santo, Danny Lyanga, Crispian Odula, Haruna Moshi ‘Boban’, Yayo Kato/Mtindi na Kenneth Masumbuko/Mohamed Athuman.
Mbali na mechi ya Tanga, mkoani Pwani, Mbeya City ililazimisha sare ya bao 1-1 na Ruvu Shooting. Bao la Ruvu lilifungwa dakika 4 na Lambele Reuben ambaye alimpiga chenga kipa wa Mbeya City, Ramadhani Abdi.
Dakika 14 Mbeya City walifuta aibu kupitia kwa Deus Kaseke akimalizia mpira uliotemwa na kipa Abdallah Abdallah aliyepigiwa shuti la haja na Paul Nonga.
Kwenye Uwanja wa Azam Complex, Azam iliifunga Rhino Rangers bao 1-0 lililopachikwa wavuni na Kipre Tchetche dakika 26 kwa mguu wa kushoto akimalizia pasi ya Mohamed Kone ambaye anazungumza Kifaransa tu. Kagera Sugar na Mtibwa Sugar zilitoka suluhu mjini Bukoba.
Katika hatua nyingine, mashabiki wanaodaiwa kuwa ni wa Yanga, wamepata ajali wakiwa safarini kuelekea mkoani Tanga kuishangilia timu yao ikivaana na Coastal Union.
Tukio hilo lilitokea maeneo ya Tange karibu na Tanga mjini jana Jumatano wakiwa kwenye gari lao aina ya Toyota Noah.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda Polisi Mkoa wa Tanga, Juma Ndaki katika ajali hiyo alikuwepo Meneja wa Bendi wa Jahazi Modern Taarab, Ally Boha ambaye amejeruhiwa.
Aliwataja wengine waliopata majeraha kuwa ni dereva wa gari hilo aliyemtaja kwa jina moja la Yasini, Kondo Karume na Mbaraka Madenga ambao wote wamepata matibabu kwenye Hospitali ya Mkoa wa Tanga, Bombo.