Yanga: pisha njia

Didier Kavumbagu aliipatia Yanga bao la pili dakika 34 baada ya kupokea pasi safi ya Msuva aliyegongeana na Mrisho Ngassa. PICHA|MAKTABA
Muktasari:
Nahodha wa Yanga, Cannavaro alisema: “Tumeshinda, imetuwezesha kuendelea na mbio za ubingwa na Azam,haikuwa mechi rahisi maana Kagera ni timu nzuri.”
YANGA inapiga tu, yaani kila anayekatiza mbele yake anaambulia kichapo na jana Jumatano ilikuwa zamu ya Kagera Sugar iliyolambwa mabao 2-1 pale Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Matokeo hayo yameifanya Yanga kubakiza pengo la pointi moja tu na vinara wa Ligi Kuu Bara, Azam FC wenye pointi 53. Unajua mashabiki wa Yanga walichokuwa wanakiimba kwa shangwe wakati wa mechi hiyo? Waliimba: “”Pi...pi...pisha njia” wakimaanisha kuwa wanataka njia ya kukwea kileleni na kumwinda mnyama Simba Aprili 19.
Hatma ya ubingwa wa Ligi Kuu Bara ilishindwa kujulikana baada ya Azam FC kushindwa kucheza na Ruvu Shooting jana Jumatano katika mchezo mwingine kati ya miwili iliyokuwa kwenye ratiba.
Azam ilikuwa ikaribishwe na Ruvu Shooting katika Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani, lakini mechi hiyo haikuchezwa kutokana na uwanja kujaa maji ya mvua kubwa iliyonyesha dakika chache kabla ya mchezo huo.
Ushindi wa Yanga umeifanya ifikishe pointi 52 hivyo kuwa nyuma ya pointi moja na Azam iliyo kileleni ikiwa na pointi 53, hata hivyo Yanga ina mechi 24 huku Azam ikiwa na mechi 23. Hii ina maana, bado mashabiki wa Yanga wataendelea kuiombea dua mbaya Azam ili ipoteze mechi yake na Ruvu Shooting ambayo sasa imepangwa kuchezwa leo Alhamisi uwanjani hapo na ile dhidi ya Mbeya City ya wikiendi hii ili mambo yawaendee vizuri wao.
Kagera imebaki nafasi ya tano ikiwa na pointi 34 baada ya kucheza mechi 24.
Yanga ilipata bao lake la kwanza dakika ya tatu lililofungwa na Hamis Kiiza aliyemalizia pasi ya Simon Msuva. Kuingia kwa bao hilo kuliongeza kasi ya mchezo katika dakika hizo za mwanzoni.
Kagera ilitafuta bao la kusawazisha ikiwatumia washambuliaji; Adam Kingwande na Paul Ngwai, lakini hawakufurukuta mbele ya safu ya ulinzi ya Yanga iliyokuwa chini ya Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Mbuyu Twite.
Didier Kavumbagu aliipatia Yanga bao la pili dakika 34 baada ya kupokea pasi safi ya Msuva aliyegongeana na Mrisho Ngassa. Bao hilo liliwavuruga Kagera kwa dakika chache kabla ya kutulia na kufanya shambulizi kali dakika 37 kwa George Kavila kupiga shuti kali lililopanguliwa na kipa wa Yanga, Deo Munishi ‘Dida’ na kuwa kona ambayo iliokolewa na mabeki wa Yanga.
Kipindi cha pili Yanga waliingilia kwa kufanya mashambulizi ya kushitukiza lakini kosa la beki wake Oscar Joshua dakika 62 la kurudisha mpira kwa kichwa hafifu kwa kipa Dida kiligharimu timu hiyo kwani Daudi Jumanne wa Kagera aliuwahi mpira huo na kufunga kirahisi.
Bao hilo liliwaamsha Kagera na kulishambulia lango la Yanga kama nyuki, lakini nguvu yao haikudumu kwa muda mrefu na walipunguza kasi dakika ya 70 na kuifanya safu ya ushambuliaji ya Yanga kucheza muda mwingi katika lango la Kagera.
Mabadiliko ya Kocha Hans Van Der Pluijm ya kumtoa Ngassa na kumwingiza, Hussein Javu, yalibadili mchezo kwa kiasi fulani na kuifanya Yanga itawale.
Safu ya ushambuliaji ya Kagera iliimarika dakika ya 84 baada ya kuingia Hamis Kitagenda aliyechukau nafasi ya Themi Felix, lakini mara nyingi hawakuwa wakipiga mashuti langoni kwa Yanga licha ya kuingia mara kadhaa katika eneo la hatari.
Nahodha wa Yanga, Cannavaro alisema: “Tumeshinda, imetuwezesha kuendelea na mbio za ubingwa na Azam, haikuwa mechi rahisi maana Kagera ni timu nzuri.”
Naye nahodha wa Kagera, George Kavila alisema: “Bado waamuzi ni tatizo katika soka la Tanzania, tutaendelea kupambana katika mechi zilizobaki.”
Yanga: Dida, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mbuyu Twite, Frank Domayo, Simon Msuva, Hassan Dilunga, Didier Kavumbagu, Mrisho Ngassa na Hamis Kiiza.
Kagera Sugar: Agathony Anthony, Salum Kanoni, Mohamed Hussein, Ernest Mwalupani, Maregesi Mwangwa, George Kavila, Benjamini Asukile, Daudi Jumanne, Adam Kingwande, Themi Felix na Paul Ngwai.
Mvua yaizuia Azam
Katika mechi iliyokuwa izikutanishe Azam na Ruvu JKT, wakati timu zikitoka vyumbani saa 9:30 alasiri, ghafla mvua kubwa ikanyesha na uwanja kujaa maji, hivyo timu zikashindwa kuendelea na zoezi la kupasha misuli moto.
Baada ya hali hiyo, mwamuzi Isihaka Shirikisho wa Tanga aliwaita manahodha na viongozi wa timu zote na kujadiliana nao kwa muda kisha kukubaliana kuahirisha mchezo huo hadi leo Alhamisi. Kutokana na hali hiyo, Azam waliamua kutorejea Dar es Salaam, badala yake walienda Kibaha kuweka kambi ya muda. Matokeo ya mchezo wao yatatoa picha ya harakati za ubingwa kwa Azam.