Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga wafanya vitu saa tatu, yaifumua Chipukizi ya Pemba

Katika mazoezi ya jana Jumatano asubuhi, wachezaji wote waliamkia ufukweni kujiweka fiti kama Simba wanavyofanya kwenye Ufukwe wa Kigamboni.

Muktasari:

  • Bao la kwanza katika mchezo huo lilifungwa na Jerry Tegete kabla ya Abdallah Mguhi ‘Messi’ kufunga la pili katika mechi ambayo Yanga ilitumia wachezaji wengi wa kikosi cha pili.

BAADA ya kuifunga Chipukizi ya Pemba mabao 2-1 jana Jumatano, Kocha wa Yanga, Ernest Brandts, amewatuliza mashabiki wa timu hiyo akiwaambia kwamba mambo yanakwenda sawa hivyo wasiwe na mchecheto kuhusiana na mechi dhidi ya Simba.

Kuthibitisha hilo jana Jumatamo aliwakimbiza wachezaji wake kwenye mchanga wa ufukweni kwa saa tatu mfululizo huko Pemba, ambako wameweka kambi kabla ya jioni yake kuifunga mabao 2-1 timu ya Chipukizi katika mchezo wa kirafiki uliofanyika kwenye Uwanja wa Gombani.

Bao la kwanza katika mchezo huo lilifungwa na Jerry Tegete kabla ya Abdallah Mguhi ‘Messi’ kufunga la pili katika mechi ambayo Yanga ilitumia wachezaji wengi wa kikosi cha pili.

Yanga imewekwa chini ya ulinzi wa meneja maalumu wa kambi, Maneno Hussein, ambaye kazi yake ni kuhakikisha hakuna yeyote asiyehusika anayejipenyeza kuingia kambini hapo kwenye hoteli ya Samail mjini Pemba ili kuzungumza na wachezaji.

Katika mazoezi ya jana Jumatano asubuhi, wachezaji wote waliamkia ufukweni kujiweka fiti kama Simba wanavyofanya kwenye Ufukwe wa Kigamboni.

Yanga ambayo imekuwa ikibadili programu zake za mazoezi kuhakikisha inakuwa fiti kwa mechi hiyo ya Jumapili, jana jioni ilicheza na Chipukizi kwenye Uwanja wa Gombani, lakini ikatumia kikosi cha pili na kuibuka na ushindi wa 2-1..

Kikosi kilichoanza ni Deo Munishi, Juma Abdul, Oscar Joshua, Ibrahim Job, Rajab Zahor, Hamis Thabit, Simon Msuva, Nizar Khalfan, Jerry Tegete, Husein Javu na Said Bahanuzi.

Yanga iliwasili Pemba Jumatatu, mara tu ilipotua iliingia moja kwa moja uwanjani kufanya mazoezi mchana wa jua kali. Lakini siku iliyofuata yaani juzi Jumanne, ikaingia kupiga tizi kwenye Uwanja wa Gombani kwa saa mbili kuanzia saa tatu asubuhi.

Jana Jumatano ikafanya mazoezi ufukweni kuanzia saa 3 asubuhi mpaka saa 5 asubuhi.

“Hatuwezi kuidharau Simba, kwani ni moja ya timu nzuri na ndio maana inaongoza ligi, hivyo naamini wamejipanga na wamejiandaa na hata sisi tunajiandaa kwa sehemu yetu, lengo ni kuhakikisha tunapata pointi tatu katika mchezo huo,” alisema Brandts.

“Tutaikabili Simba kama timu nyingine kwenye ligi, najua utakuwa mchezo wa upinzani sana kwa sababu tunakutana timu kubwa mbili pinzani hapa nchini, lakini tusubiri dakika 90. Ila ninawaahidi mashabiki wetu watafurahia soka kutoka kwetu.

“Nimewaona Simba katika baadhi ya mechi, najua wanavyocheza kwa kila mchezaji wao, najua udhaifu wao na mbinu zao ingawa siwezi kuzitaja kwani zitabaki katika makabrasha yangu, ila nitatumia udhaifu wao kuwamaliza. “Ninachofurahi sina majeruhi, Ngassa (Mrisho) anaumwa malaria lakini anafanya mazoezi mepesi, kadiri muda unavyokwenda afya yake inazidi kuimarika, pia Telela (Salum) naye anaendelea vizuri, ninachoomba mpaka kufika siku hiyo wachezaji wote wawe fiti kwa asilimia 100.”