Yanga wanaume wa shoka

Muktasari:
- Yanga imeondolewa na Al Ahly ya Misri baada ya jana Jumapili usiku kufungwa kwa penalti 4-3 katika mchezo wa marudiano raundi ya kwanza jijini hapa.
YANGA imeondolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika lakini imepigana kiume na kudhihirisha kwamba ni Wanaume wa shoka. Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara walikomaa na kuonyesha soka safi ndani ya dakika 90 na kushangaza wengi ambao walikuwa wakiibeza.
Yanga imeondolewa na Al Ahly ya Misri baada ya jana Jumapili usiku kufungwa kwa penalti 4-3 katika mchezo wa marudiano raundi ya kwanza jijini hapa.
Awali Yanga ilikuwa imefunga bao 1-0 Al Ahly katika mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam lakini ikafungwa bao 1-0 katika marudiano jana kwenye Uwanja wa Haras El Hoodod, ndipo ilipoamuliwa mikwaju ya penalti na mwamuzi Badara Diatta wa Senegal ambaye alifuata sheria za Fifa kwani matokeo ya mechi hiyo yalilingana kwa kila kitu nyumbani na ugenini.
Kipindi cha kwanza Yanga ilicheza soka safi huku Al Ahly wakionekana kuhofu mashambulizi yao kutokana na Yanga kuwa na mawinga wenye kasi Mrisho Ngassa na Simon Msuva.
Hadi dakika 45 zinamalizika, timu hizo zilikuwa hazijafungana. Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku kila timu ikionekana kutaka bao la haraka lakini safu za ulinzi zilikuwa makini kuokoa hatari zote.
Mabadiliko ya kumtoa Ngassa na kuingia Athuman Idd ‘Chuji’ yalipoozesha mashambulizi ya Yanga, kwani hakukuwa na nguvu kubwa ya kushambulia pembeni hivyo Al Ahly wakaanza kushambulia kwa nguvu kutumia upande wao wa kushoto.
Al Ahly iliamka na kufanikiwa kupata bao dakika ya 71 lililofungwa na Sayed Mouwad baada ya kumalizia mpira uliorudi baada ya shambulizi kali langoni kwa Yanga ambayo ilikuwa ikishambulia kwa kujiamini.
Al Ahly walicharuka baada ya kuingia kwa bao hilo na kulishambulia lango la Yanga kama nyuki na kukosa mabao kadhaa ya wazi dakika za 80 na 86. Hadi dakika ya 90, Yanga ilikuwa nyuma kwa bao 1-0.
Katika penalti, Yanga ilipata mikwaju mitatu iliyopigwa na Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Didier Kavumbagu na Emmanuel Okwi wakati Oscar Joshua, Said Bahanuzi na Mbuyu Twite walikosa.
Dakika ya 60, Dida aliwavuruga kisaikolojia wachezaji wa Al Ahly kwa kufanya kama anaweka vitu visivyoeleweka langoni kwake na kuzua sintofahamu kwa wapinzani wao.
Hata hivyo kipa huyo alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 61 na mwamuzi Badara Diatta wa Senegal kwa kosa la kuchelewesha muda.
Wakati huohuo, kabla ya kuingia katika vyumba vya kubadilishia nguo katika Uwanja wa El Max, viongozi wa Yanga waliwazuia wachezaji wa timu hiyo kuingia vyumbani baada ya kugundua hewa nzito wakihofu kupulizwa kwa dawa za kupunguza kasi.
Viongozi wa Yanga walitangulia kuingia katika vyumba hivyo kubaini hali hiyo ndipo walipowakataza wachezaji wao kuingia ndani na kulazimika kubadili nguo zao katika basi lililowapeleka uwanjani hapo.
Hata hivyo baada ya kutoka kupasha misuli moto, viongozi waliwaruhusu kuingia katika vyumba hivyo baada ya kujiridhisha na hali ya hewa iliyokuwepo baada ya kufungua masinki ya maji ili kutoa hewa chafu.
Hivyo ni baadhi tu ya vituko walivyokutana navyo Yanga kuelekea mchezo wao wa jana lakini vingi vilishtukiwa na viongozi wa timu hiyo waliokuwa makini katika kila hatua ya kuelekea katika mechi hiyo.
Al Ahly sasa itacheza na mshindi wa mechi kati ya Berekum Chelsea ya Ghana na Al Ahly Benghaz ya Libya.
Yanga iliwakilishwa na Deo Munishi ‘Dida’, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Frank Domayo, Mrisho Ngassa, Didier Kavumbagu, Emmanuel Okwi, Hamis Kiiza na Simon Msuva.