Yanga ya Kizungu Uturuki

Kocha Kopunovic Goran kutoka Serbia
Muktasari:
- Mwanaspoti linaweza kuthibitisha kwamba mpaka jana Jumatano usiku, Yanga ilikuwa ikifanya mazungumzo ya karibu sana na makocha wawili; Mbelgiji, Luc Eymael na Mserbia Kopunovic Goran huku ikitaka kusikiliza ofa zao kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho.
YANGA imethubutu na imeweza. Kwa mara ya pili mfululizo itatua kwenye mji wa Antalya, Uturuki mchana wa leo Alhamisi kuweka kambi ya wiki mbili kujiandaa na Ligi Kuu Bara mzunguko wa pili na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Si hilo tu, Mwanaspoti linaweza kuthibitisha kwamba mpaka jana Jumatano usiku, Yanga ilikuwa ikifanya mazungumzo ya karibu sana na makocha wawili; Mbelgiji, Luc Eymael na Mserbia Kopunovic Goran huku ikitaka kusikiliza ofa zao kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho.
Luc na Goran ni miongoni mwa makocha 50 kutoka nchi mbalimbali walioomba kazi ya kuinoa Yanga baada ya kutimuliwa kwa Mholanzi, Ernest Brandts na benchi lake.
Luc na Goran wameomba kazi ya kuwa makocha wa Yanga.
Goran, ambaye alikuwa Kocha wa Police FC ya Rwanda kwa miaka mitatu alifanya maajabu na kuiwezesha timu hiyo ambayo ilikuwa ya kawaida kuwa tishio Ligi Kuu Rwanda.
Goran, alikuwa Kocha wa Police FC ya Rwanda kuanzia mwaka 2010 mpaka msimu uliopita alipotimuliwa baada ya kuifanya timu hiyo kushika nafasi ya pili.
Habari za ndani kutoka kwenye kikao cha Yanga kilichofanyika jijini Dar es Salaam zinasema kwamba mabosi hao walikuwa wakijadiliana kuhusu ofa ya Luc na Goran ambao kati yao mmoja ana nafasi kubwa ya kuja Yanga.
Luc yupo Ubelgiji na Goran yupo Serbia na kila mmoja ambaye amewaambia Yanga kwamba yupo tayari kujiunga na timu hiyo moja kwa moja kambini mjini Antalya.
Angani
Yanga imeondoka jijini Dar es Salaam saa 10:35 alfajiri leo Alhamisi na ndege ya Uturuki ‘Turkish Airline’ na itakaa angani kwa muda wa saa sita kabla ya kutua Istanbul ambao ni mji mkuu wa Uturuki saa 4:50 asubuhi.
Ikishatua Instanbull italazimika kusubiri uwanjani hapo hadi majira ya saa 7:30 mchana ili kupata ndege ya kuunganisha kwenda mjini Antalya ambako ni umbali wa saa moja na itawasili huko saa 8:45 mchana.
Hali ya Hewa
Mji huo ambao hoteli za fukwe na viwanja vya kisasa vyenye utulivu wa hali ya juu, kuna hali ya hewa ya baridi ingawa timu kutoka mataifa mbalimbali hupenda kuweka kambi maeneo hayo majira haya.
Hali ya hewa ya Antalya kwa sasa majira ya mchana ni nyuzi joto 16 mpaka 18 ambapo usiku hushuka mpaka nyuzi joto 5 ikiambatana na upepo mkali ambapo huwezi kutembea hata mchana bila kuvaa koti.
Gharama za ndege kufikia Antalya na kurudi ni Dola 1,128 ambayo ni sawa na Sh.1.7 milioni kwa kichwa kimoja ambapo Yanga italazimika kulipa Sh 58 Milioni kwa msafara wa watu wake 33.
Msafara
Yanga inaondoka na msafara wa watu 33, kati yao wachezaji ni 27 viongozi wakiwa sita, wakielekea katika mji wa Antalya ambako waliwahi kuweka kambi msimu uliopita.
Wachezaji watakaondoka ni makipa Juma Kaseja, Deogratias Munishi ‘Dida’ na Ally Mustapha ‘Barthez’. Mabeki ni Mbuyu Twite, Kelvin Yondani, Ibrahim Job, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Juma Abdul, David Luhende, Rajab Zahir, Oscar Joshua, viungo ni Frank Domayo, Hassan Dilunga, Haruna Niyonzima, Bakari Masoud, Hamis Thabit, Simon Msuva, Nizar Khalfan.
Washambuliaji ni Shaaban Kondo, Said Bahanuzi, Mrisho Ngassa, Jerry Tegete, Hussein Javu, Hamis Kiiza, Didier Kavumbagu, Reliants Lusajo na Emanuel Okwi.
Walioachwa ni Salum Telela ambaye ni mgonjwa, Athuman Idd ‘Chuji’ aliyesimamishwa na makinda Abdallah Mguhi ‘Messi na kipa Yusuf Abdul.
Viongozi watakaombatana na timu hiyo ni pamoja na mkuu wa msafara ambaye ni mjumbe wa kamati ya utendaji Salum Rupia, makocha Charles Boniface Mkwasa, Juma Pondamali, Daktari Juma Sufiani, Ofisa Habari, Baraka Kizuguto na meneja wa timu, Hafidh Saleh.