Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga yafikiria mbadala wa Yao, Keita atajwa

Muktasari:

  • Yao, maarufu kwa jina la Jeshi alianza kupona, lakini inaelezwa amepata majanga mengine eneo aliumia awali ambapo huenda akakaa nje kwa muda zaidi.

MASHABIKI wa Yanga hawajamuona uwanjani beki wao Yao Kouassi, kwa muda sasa akipambana kurudi uwanjani kutoka kwenye majeraha ya nyama za paja, lakini hatua hiyo inawavuruga zaidi mabosi wakiwa na hesabu kali.

Yao, maarufu kwa jina la Jeshi alianza kupona, lakini inaelezwa amepata majanga mengine eneo aliumia awali ambapo huenda akakaa nje kwa muda zaidi.

Yanga inasubiri ripoti ya madaktari wa klabu kufahamu mchezaji huyo atakuwa nje kwa muda gani, lakini nyuma yake kuna hesabu mpya zinapigwa juu ya beki mmoja wa kazi kutoka TP Mazembe ya DR Congo.

Endapo Yao atashindwa kuwahi kurudi licha ya kuonekana anajaribu kuchezea mpira mazoezini, Yanga itamshusha beki Ibrahima Keita, raia wa Mauritania.

Hesabu za Keita na Yanga hazijaanza sasa, kwani beki huyo jina lake kwa mara ya kwanza lilitua Jangwani tangu Kocha Nasredine Nabi anainoa timu hiyo, ambaye alitaka kumsajili kama angebaki kabla ya Julai 17, 2023 kutimka FAR Rabat ya Morocco.

Baada ya Nabi kuondoka, Yanga ikamsajili Yao kuchukua nafasi ya Mkongomani, Djuma Shaban, huku Keita akitua TP Mazembe akitokea Bobigny U19 ya Ufaransa.

Chanzo cha ndani kimeliambia Mwanaspoti kuwa, “Yao kwa kweli maisha yake msimu huu wa pili si mazuri, amekumbana na janga la majeraha, hivi karibuni tuliona kama amepona, lakini ghafla amerejea tena kwenye majeraha na sidhani kama tutamuona uwanjani tena msimu huu.

“Ilikuwa tumalizane na yeye, lakini tunataka kwanza kupata ripoti kamili juu ya muda gani atakuwa nje halafu tutafanya uamuzi wa kipi kifanyike kwake.

“Hakuna asiyejua uwezo wa Yao akiwa sawa, huyu ni jeshi hasa kama ambavyo mashabiki wanamuita, inatuumiza kwa anayoyapitia lakini ndio soka.”

Pale TP Mazembe, Keita ameshawaga mabosi wa klabu hiyo akiwagomea katakata kuongeza mkataba ambao unamalizika mwezi ujao, huku Yanga na Kaizer Chiefs inayofundishwa na Nabi zikiwa zinavizia huduma yake kwa ajili ya msimu ujao.

Msimu huu kwenye ligi, Yao amecheza mechi saba kati ya 26 ambazo Yanga imecheza, huku akiwa hana rekodi ya kufunga bao wala kutoa asisti.


HALI ILIVYO

Mikakati ya Yanga hivi sasa ni kuboresha kikosi chao mapema kuelekea msimu ujao ambapo ndani ya klabu hiyo kuna taarifa za baadhi ya nyota kuwa mbioni kuuzwa na wengine kuachana nao baada ya mikataba kufikia ukomo mwisho wa msimu.

Djigui Diarra na Stephane Aziz Ki inaelezwa kuna timu zinawataka, hivyo Yanga ina mpango wa kufanya biashara ya kuwauza, huku Khalid Aucho, Kennedy Musonda, Clatous Chama, Jonathan Ikangalombo na Yao Kouassi Attohoula mikataba inamalizika ilhali kukiwa na majadiliano ya kuongeza au kuachana nao wakati Salum Abubakar ‘Sure Boy’na Farid Musa wapo kwenye mipango ya kupelekwa Singida Black Stars kwa mkopo.


WANAOFUKUZIWA

Mbali na Keita, nyota wengine waliopo kwenye rada za Yanga ni Josaphat Arthur Bada (Singida Black Stars), Koimizo Maiga (Asec Mimosas), Jonathan Sowah (Singida Black Stars), Feisal Salum (Azam), Henock Inonga (AS FAR Rabat), Mohammed Omar Ali Bajaber (Kenya Police), Amas Obasogie (Singida Black Stars).

Hivi karibuni, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, alisema: “Wachezaji bora wengi lazima uanze kuwatafuta mapema, kama mchezaji yupo huru maana yake mkataba wake unaelekea kumalizika na yule mwenye mkataba mazungumzo na klabu yake yanaanza kipindi hiki.

“Tumeanza kuboresha timu yetu kwa ajili ya msimu ujao - maboresho ya kwanza ni kubakisha nyota tulionao kwa mujibu wa ripoti ya mwalimu. Wale ambao watataka kuondoka tutaangalia kwa maslahi ya klabu nani tumuondoe, lakini malengo makubwa ni kutengeneza timu ya msimu ujao kwa sababu tayari tuna tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa.”

Mwanaspoti pia limewahi kuripoti kuwa Kocha wa Yanga ambaye anatajwa anaondoka mwisho wa msimu huu, Miloud Hamdi, amewasilisha mapendekezo ya maboresho ya kikosi hicho kwa namna alivyoona tangu aanze kukifundisha Februari mwaka huu.

Hamdi ameyataja maeneo manne ya kuboreshwa ambayo ni mshambuliaji wa mwisho, namba 10, beki wa kati na kiungo mkabaji.