Yanga yaishtukia Simba, wachezaji 15 wapo sokoni

Kiungo mkabaji wa Timu ya Yanga Athuman Iddy 'Chuji' akifafanua jambo wakati wa mazoezi siku za hivi karibuni. Picha na Maktaba
Muktasari:
- Huenda wachezaji hao wakasaini Yanga haraka kabla hata Kilimanjaro Stars haijaondoka keshokutwa Jumatatu kwenda Kenya kwenye michuano ya Kombe la Chalenji.
WACHEZAJI 15 wa mabingwa wa soka nchini, Yanga wapo sokoni kutokana na mikataba yao kubakiza miezi sita tu, lakini Yanga wameshitukia dili na wanachotaka kufanya kwanza ni kuwasainisha mikataba wachezaji watatu.
Huenda wachezaji hao wakasaini Yanga haraka kabla hata Kilimanjaro Stars haijaondoka keshokutwa Jumatatu kwenda Kenya kwenye michuano ya Kombe la Chalenji.
Kikanuni wachezaji hao wanaruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu yoyote ile na kusaini ndio maana Yanga wameshituka kwamba wapinzani wao ikiwemo Simba na maskauti wengine wanaweza kutua Kenya na kuwasainisha mastaa wake.
Hivyo Yanga walichofanya ni kuwadhibiti kwanza wachezaji watatu kati ya hao 15. Wachezaji hao ni Athumani Idd ‘Chuji’, Frank Domayo na Kelvin Yondani.
Chanzo cha kuaminika kutoka Yanga kiliiambia Mwanaspoti jana Ijumaa kwamba uongozi wa klabu hiyo upo katika mikakati ya kuhakikisha baadhi ya wachezaji hao ambao bado wako katika viwango vya juu wanasainishwa mapema.
Wachezaji ambao kwa sasa wanaweza kufanya mazungumzo na klabu yoyote kwa mujibu wa kanuni za Fifa ni pamoja na kipa Ali Mustapha ‘Barthez’ ambaye nafasi yake katika timu hiyo kwa sasa ipo katika hatihati baada ya kusajiliwa kipa nyota nchini, Juma Kaseja.
Wengine ni beki kisiki kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, MbuyuTwite, Juma Abdul, David Luhende, Nadir Haroub, Ibrahim Job na Kelvin Yondani.
Kwa upande wa viungo ni Chuji, Domayo, Said Bahanuzi, Simon Msuva, Salum Telela na Nizar Khalfan na washambuliaji ni Didier Kavumbagu na Jerryson Tegete.
Habari za ndani zinadai viongozi Yanga wamekuwa wakiumiza vichwa kuhusu wachezaji hao na kuanzia wikiendi hii baadhi yao wataanza kusaini ili wasichukuliwe na timu nyingine.
“Mazungumzo na wachezaji hao yanaendelea na tunaamini mpango wa kuwabakiza utakamilika, lakini kimsingi hali ndiyo hiyo ndani ya klabu yetu,” kilisema chanzo chetu na kusisitiza kwamba wanataka kuondoa utata huo ili waingie kamili kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.
“Kuna wachezaji ambao wataondoka na timu ya Taifa kwenda Nairobi kwa ajili ya mashindano ya Chalenji, ni muhimu wachezaji hao kusaini mkataba mpya kabla ya safari, maana Kenya lolote linaweza kutokea kwani kuna maskauti kibao na wanaweza kuingia vishawishi,” alisema.
Alisema kuwa wachezaji ambao mpaka sasa wana mikataba ya muda mrefu na inayozidi miezi sita ambao ni Hamis Kiiza, Deogratius Boniventura Munishi, Haruna Niyonzima, Oscar Joshua, Rajab Zahir, Relaint Lusajo, Shaban Kondo, Hussein Javu, Mrisho Ngassa, Yusuph Abdul, Hamis Thabit na waliosajiliwa hivi karibuni, Juma Kaseja na Hassan Dilunga.
Taarifa za ndani ni kwamba wachezaji kama Job na Bahanuzi watapelekwa kwa mkopo Ruvu JKT ili kuangalia viwango vyao. Kocha wa Ruvu JKT, Mbwana Makatta alikiri kupeleka maombi hayo kwa Yanga.
Akizungumzia hatma yake Yanga, Chuji alikiri kubakiza muda huo mchache katika klabu hiyo huku akisema kuwa suala la kusaini mkataba mpya itategemea na makubaliano.
“Namalizia muda wangu ndani ya klabu, lakini siwezi kusema kama nitahama au la, hilo litategemea makubaliano,” alisema.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Yanga, Abdallah Bin Kleb alisema kuwa wao wanafanya mambo yao kwa siri na hawawezi kuweka bayana nani anasajili wachezaji wapya na wale ambao wanaitumikia klabu mpaka sasa.
“Wiki ijao tutakuwa na nafasi ya kusemea hayo, kwa sasa bado kwani tuna mikakati ya kuiongezea nguvu timu, mara nyingi hatutaki kusema kitu kabla ya kukamilika, tunakamilisha na baadaye tunatangaza kikiwa kamili,” alisema Bin Kleb.