Yanga yaitungua Mbeya City, Azam yafanya kufuru

Wachezaji wa Yanga wakishangilia bao lililofungwa na Mrisho Ngassa dhidi ya Mbeya City. Yanga ilishinda 1-0. Picha na Michael Matemanga
Muktasari:
- Wanaume hao ni Azam Fc na Mbeya City, lakini mambo yamebadilika. Kwa mara ya kwanza Mbeya City imepoteza mechi baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Yanga jana Jumapili jioni kwenye Uwanja wa Taifa.
TANGU kuanza kwa Ligi Kuu Bara msimu wa 2013/14 kuna wanaume wawili tu waliokuwa hawajapoteza mechi yoyote kwenye Ligi.
Wanaume hao ni Azam Fc na Mbeya City, lakini mambo yamebadilika. Kwa mara ya kwanza Mbeya City imepoteza mechi baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Yanga jana Jumapili jioni kwenye Uwanja wa Taifa.
Mechi ambayo iliwaweka kwenye wakati mgumu wachezaji wa Mbeya City iliyokuwa na sapoti kubwa ya Simba kwani baada ya mchezo huo wachezaji na mashabiki wa Yanga walikuwa wakiwaonyesha ishara za vidole wakimaanisha “kaeni kimyaa hii ndiyo Yanga Afrika”.
Ushindi wa Yanga umeipa pointi 35 ikatulia kwenye nafasi ya pili, baada ya Azam kuikung’uta bila huruma Kagera Sugar mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi. Azam imetimiza pointi 36 huku Mbeya City ikiendelea kushika nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi 31 wakati Simba ni ya nne ikiwa na pointi 27.
Yanga walionekana kuishambulia kwa umakini Mbeya City ingawa vijana hao wa Mbeya hawakukata tamaa na walionyesha kujiamini na walicheza kwa nguvu jambo ambalo mara kadhaa liliwatisha Yanga.
Sekunde la 48, Simon Msuva alipoteza nafasi ya wazi baada ya kupiga shuti lililopaa juu akipokea pasi ya Oscar Joshua wakati wapinzani wao Mbeya City nao wakikosa bao la wazi dakika 13 baada ya mchezaji wao Paul Nonga kupiga shuti ndefu na mpira kutoka nje akitumia makosa ya Kelvin Yondani.
Mrisho Ngassa wa Yanga alifunga bao pekee na la ushindi kwenye mchezo huo dakika 16, akipiga shuti kuunganisha mpira wa kichwa uliopigwa na beki wa Mbeya City, Yusuf Abdallah aliyekuwa akiokoa krosi safi ya David Luhende.
Yanga walionekana kulishambulia kwa nguvu lango la Mbeya City huku Mwagane Yeya akipoteza nafasi dakika 24 baada ya kupiga mpira kwa kichwa na kushindwa kulenga lango akipokea krosi ya Kaseke.
Luhende alipoteza nafasi ya wazi dakika 27 baada ya kupiga shuti ndefu na mpira kutoka nje akipokea pasi safi ya Didier Kavumbagu, dakika 31 kipa wa Yanga Deo Munishi ‘Dida’ aliokoa hatari iliyotokana na krosi ya Peter Mapunda iliyokuwa ikisubiriwa na Yeya tayari kwa kufunga.
Bahati haikuwa ya Nonga kwani dakika 35 pia alipoteza nafasi ya kuipatia bao timu yake baada ya shuti lake kupanguliwa na Dida huku dakika ya 41 Nonga akiinyima tena timu yake bao la wazi kwani shuti lake lilitoka nje kidogo baada ya kupokea pasi safi ya Mapunda aliyemkimbiza vibaya Oscar Joshua winga ya kulia.
Kipindi cha pili Mbeya City ilipata pigo baada ya kiungo wake Mazanda kupewa kadi nyekundu baada ya kutoka kwenye mstari kabla ya mpira kupigwa wakati Yanga ikitaka kupiga mpira wa adhabu baada ya Hassan Mwasipili kuunawa mpira na mwamuzi Abdallah Kambuzi kuampa kadi nyekundu.
Dakika 61 Kocha wa Yanga, Hans Van Der Pluijm alifanya mabadiliko, alimtoa Mbuyu Twite na kumuingiza Juma Abdul alimtoa Didier Kavumbagu dakika 64 nafasi yake ilichukuliwa na Hamis Kiiza.
Kocha wa Mbeya City, Juma Mwambusi, naye alifanya mabadiliko kwa kumtoa Nonga ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Richard Peter dakika 64.
Kiiza aliikosesha bao timu yake dakika 65 baada ya kuchelewa krosi iliyopigwa na Ngassa huku Msuva akikosa bao dakika 67 shuti lake likienda nje kidogo ya lango.
Mwambusi alifanya mabadiliko tena dakika 71 kwa kumtoa Deus Kaseke aliyekuwa akisumbuliwa na mabeki wa Yanga nafasi yake ilichukuliwa na Joseph Wilson na dakika 72 Mbeya City walipoteza nafasi baada ya mpira wa adhabu ndogo iliopigwa kwa ufundi mkubwa pasi ikawa ndefu kidogo kwa Yeya aliyeruka kwa kichwa.
Dakika 74, Kiiza akiwa pekee yake na kipa alikosa bao baada ya mpira aliomnyanyulia kipa David Burhan kushindwa kulenga lango.
Mwambusi aliamua kufanya mabadiliko dakika 75 akimtoa Yeya na kumwingiza Saad Kipanga.
Kiiza aliipatia Yanga bao la pili dakika 79 alilofunga kwa kichwa lakini mwamuzi alilikataa bao hilo akidai mfungaji aliotea wakati mashabiki wa Yanga wakiwa tayari wameamka kwenye viti vyao na kuanza kushangilia.
Zikiwa zimesalia dakika tatu za nyongeza, kiungo wa Yanga aliyekuwa amesimamishwa Athuman Idd ‘Chuji’ aliingia uwanjani akiwa amevaa nguo za kawaida huku akiwapungia mkono mashabiki ambao pia walimjibu kwa kumshangilia.
Chuji hakuishia hapo aliendelea kuonyesha matendo kwa mashabiki wake ikiwa ni ishara ya kuwaomba msamaha na baada ya mechi kumalizika aliwafuata wachezaji wenzake na kuwakumbatia pamoja na makocha wake.
Akizungumzia mechi hiyo, kocha wa Yanga Pluijm, alisema kuwa wamepata nafasi nyingi ila wachezaji wake walishindwa kuzitumia na kudai kuwa wachezaji wa Mbeya City wana nguvu na kuahidi kuwapa mazoezi kama hayo wachezaji wake.
Kwa upande wa kocha wa Mbeya City, Mwambusi, alisema kuwa mechi ilikuwa ngumu ingawa hajawahi kucheza timu yake ikiwa pungufu tangu aingie kwenye ligi baada ya mchezaji wake kupewa kadi nyekundu.
Mwambusi alisema mwamuzi hakupaswa kumpa kadi hiyo mchezaji wake Mazanda wakati anatambua ana kadi ya njano hivyo alitakiwa kumuonya, aliongeza kuwa waamuzi ndiyo wanaoharibu mechi.
Katika hali isiyo ya kawaida, straika wa Yanga aliyekosa namba hata kwenye benchi, Shaaban Kondo alikamatwa na polisi uwanjani hapo na kupigwa pingu alipokuwa akiingia vyumbani kwenda kuwapongeza wenzake. Mmoja wa askari alidai kwamba mchezaji huyo alitumia lugha chafu na tayari wamemfungulia kesi ya uvunjifu wa amani.
Kikosi cha Yanga: Deo Munishi ‘Dida’, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Frank Domayo, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Didier Kavumbagu, Mrisho Ngassa na David Luhende.
Mbeya City: David Burhan, John Kabanda, Hassan Mwasapili, Deogratius Julius, Yusuf Abdallha, Anthony Matogolo, Mwagane Yeya, Steven Mazanda, Paul Nonga, Peter Mapunda na Deus Kaseke.
Azam vs Kagera
Azam jana iliendelea kubaki kileleni baada ya kuifunga Kagera Sugar mabao 4-0.
Mabao ya Azam yalifungwa na Briany Umony aliyefunga mawili dakika za 10 na 48, bao la tatu lilifungwa na Kelvin Friday dakika 51 wakati bao la nne lilifungwa na Jabir Aziz dakika 82
Wachezaji wa timu zote walicheza kwa kushambuliana ingawa Kagera Sugar walikuwa na tatizo katika safu ya umaliziaji.
Azam ilimtoa Kamwaga dakika 21 baada ya kuumia na nafasi yake ilichukuliwa na Kelvin Friday, Kagera Sugar ilitawala mchezo kipindi cha kwanza kusaka goli la kusawazisha lakini mabeki wa Azam walionekana kuwa imara kulinda lango lao.
Azam FC: Mwadin Ally, Erasto Nyoni, Malika Philipo, Said Morad, Aggrey Moris, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Kipre Balou, Himid Mao, Joseph Kimwaga/Kelvin Friday, Kipre Chetche/Gaudence Mwaikimba na Brian Umony.