Yanga yamtuma kocha Mkwasa Misri

Muktasari:
- Kwa mujibu wa Seif Ahmed ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Kimataifa wa Yanga, watamtuma Mkwasa, kuiona Al Ahly ikicheza mechi hiyo muhimu.
YANGA imemtuma kocha wake msaidizi, Boniface Mkwasa nchini Misri kuangalia mechi baina ya Al Ahly na Safaxien ya Tunisia kwenye mechi maalum ya Super Cup itakayochezwa kesho kutwa Alhamisi mjini Cairo. Kwa mujibu wa Seif Ahmed ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Kimataifa wa Yanga, watamtuma Mkwasa, kuiona Al Ahly ikicheza mechi hiyo muhimu.
Seif alithibitisha kwamba Mkwasa ataondoka kesho Jumatano. Kocha Pluijm alithibitisha kwamba wanazo CD za Ahly, lakini ni za kipindi cha nyuma.
Kocha wa Yanga, Hans Van Der Pluijm, amesema anajua Al Ahly wanatumia mawinga kushambalia, hivyo analazimika kubadili haraka mfumo wa kuzuia wa timu yake hivyo ataimarisha pia viungo kushambulia.
Akizungumza na Mwanaspoti jana Jumatatu mjini hapa kabla ya kurudi Tanzania na timu yake, Pluijm alisema analazimika kuisuka upya kiufundi na kuipa majukumu maalumu safu ya ulinzi.
Mabeki tegemeo wa Yanga ni Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani wanaocheza katikati, kushoto anapiga Oscar Joshua huku kulia akisimama Mbuyu Twite.
“Najua wanatumia sana winga kushambulia kuliko katikati, hivyo lazima mabeki wangu wawe makini kuzuia kuanzia mbele ili kutowapa nafasi ya kutushambulia kirahisi, nitawaongezea kitu cha kufanya mabeki wangu,” alisema kocha huyo.
“Hata katika ushambuliaji, narekebisha kitu kwani katika mechi yetu ya Moroni hawakupata pasi nyingi za mwisho ndiyo maana hawakufunga mabao mengi, hivyo kabla ya kuivaa Al Ahly natakiwa kufanya kitu fulani ili tubadilike.”
Habari za ndani zinadai kuwa kocha huyo amewaambia viongozi kwamba atajitoa muhanga kuweka rekodi na Yanga.
Alisema katika mchezo dhidi ya Komorozine, mshambuliaji mmoja wa Yanga alilazimika kucheza kama kiungo mshambuliaji ili kuwalisha mipira washambuliaji wenzake.
“Sijui kwa nini wanaweza kufanya vizuri katika mazoezi, lakini mechi kama wakiiona nyepesi wanacheza kwa kutulia na kujisahau sasa sijui inakuaje, nitawaeleza wabadilike,” alisema.