Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga yatakata Dar, Simba yabanwa

Wachezaji wa Yanga wakishangilia baada ya kuifunga Rhino Rangers ya Tabora kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana Jumatano. Picha na Michael Matemanga.

Muktasari:

Mechi za jana Jumatano zilikuwa na hisia ya aina yake kwani Simba na Yanga zilitaka kushinda kwa kishindo kurudisha morali iliyopotea baada ya sare yao ya mabao 3-3 wikiendi iliyopita ndani ya Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

YANGA ikipukutisha mastaa wake wengi wa kikosi cha kwanza, iliichapa Rhino Rangers mabao 3-0 huku Simba ikishindwa kuishusha Azam kwenye usukani wa Ligi Kuu Bara.

Mechi za jana Jumatano zilikuwa na hisia ya aina yake kwani Simba na Yanga zilitaka kushinda kwa kishindo kurudisha morali iliyopotea baada ya sare yao ya mabao 3-3 wikiendi iliyopita ndani ya Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Yanga ambayo mabao yake yalifungwa na Hamis Kiiza mawili na moja la Frank Domayo dhidi ya Rhino Rangers imefikisha pointi 19 ikizidiwa pointi moja na Simba, Azam na Mbeya City zilizobanana nafasi tatu za juu kwa tofauti ya mabao.

Vijana hao wa Jangwani katika kikosi cha kwanza cha jana Jumatano iliwaanzisha Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, David Luhende/Oscar Joshua, Mbuyu Twite, Kelvin Yondani, Rajab Zahir, Simon Msuva/Nizar Halfan, Frank Domayo, Hamis Kiiza, Mrisho Ngassa na Haruna Niyonzima.

Kikosi hicho cha Yanga kilionekana kutocheza soka la kuvutia kipindi cha kwanza ingawa, Rhino ambao walikuwa na wachezaji wazoefu kama Nurdin Bakary na Stanslaus Mbogo walishindwa kuonyesha cheche zao licha ya mastraika Victor Hangaya na Saad Kipanga kujitahidi kupangua uzio wa Yanga na kupiga mashuti ambayo Dida aliyaona.

Mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika Yanga ilikuwa ikiongoza kwa bao la Kiiza lililofungwa kwa shuti dakika ya 12 baada ya kupokea pasi ya Msuva na beki Julius Masunga kushindwa kuokoa.

Domayo alifunga bao pili la Yanga dakika ya 73 kwa kuunganisha pasi ya Ngassa, ambaye alikuwa akichachafya kwa kasi yake na dakika ya 81 Kiiza alifunga bao la tatu na la ushindi la Yanga ambayo kocha wake, Ernest Brandts alisema alifanya mabadiliko makusudi.

Brandts alisema: “Nimeingiza sura mpya kwenye kikosi cha kwanza ili kuleta mvuto mpya na kuona uwezo wa wachezaji ambao hawajacheza tangu ligi ianze, nimefurahia viwango vyao na ushindi ambao umetuweka kwenye nafasi nzuri.”

Rhino; Mohamed Othman, Ally Mwanyiro, Husein Abdalah, Julius Masunga, Stanslaus Mbogo, Stanslaus Mwakitosi, Shija Mongi, Iman Noel/Msafiri Hamis, Victor Hangaya, Saad Kipanga, Nurdin Bakari.

Mjini Tanga, Simba ikiwatumia Abel Dhaira/Abuu Hashim, Said Nassor ‘Cholo’/Edward Christopher, Haruna Shamte, Gilbert Kaze, Joseph Owino, Jonas Mkude, Ramadhani Singano, Said Ndemla, Amis Tambwe, Amri Kiemba/Zahor Pazi na Wiliam Lucian ilitulizwa na wenyeji Coastal Union waliokuwa na kocha wao mpya, Joseph Lazaro.

Simba ambayo ilikuwa bila ya straika wake mwenye nguvu Betram Mwombeki na msumbufu wa mabeki Haroun Chanongo, mabeki wa Coastal chini ya Juma Nyosso walimtuliza Tambwe na Amri Kiemba wasilete madhara.

Dhaira alishindwa kuendelea na mchezo huo na kutolewa mapema kipindi cha kwanza baada ya kutonesha bega aliloumizwa na Didier Kavumbagu kwenye mechi ya watani wa jadi wikiendi iliyopita.

Mechi hiyo ambayo ilijaza uwanja huo na kuuchangamsha mkoa wa Tanga ilikuwa na mashamsham ya aina yake ambapo wachezaji wa zamani wa Simba Haruna Moshi Boban, Uhuru Seleman na Juma Nyosso waliwashambulia Wekundu hao wa Msimbazi mara kadhaa huku wakihamasisha wenzao kubadili matokeo lakini ikashindikana.

Kocha Msaidizi wa Simba, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ alisema: “Sare si mbaya kwetu kwavile tutakuwa sawa na Azam ambayo tukicheza nayo mchezo unaofuata tukiwafunga tunashika usukani wa ligi, Coastal Union imetubana kwavile ilikuwa na wachezaji wazoefu na ilitaka kushinda kwenye uwanja wao.”

Lazaro wa Coastal alijitetea kwa kusema: “Sikushinda kwavile ni mechi yangu ya kwanza, najaribu kutengeneza timu mpya, ila nashukuru kwamba hamasa imekuwa kubwa na morali ya timu imebadilika.”

Coastal; Shaaban Kado, Mbwana Hamis, Tamin Othman, Marcus Rafael, Juma Nyosso, Jerry Santo, Danny Lianga/ Uhuru Seleman, Chistopher Odulla, Yaiyo Kato, Boban na Kenneth Masumbuko.