Yanga yawaacha Kaseja, Okwi safari ya Comoro

Kocha wa Yanga, Hans Pluijm (katikati) akiwawaelekeza jambo wachezaji wake katika mazoezi yao ya jana Jumatano asubuhi katika Uwanja wa Karume, Dar es Salaam. Yanga itaondoka leo Alhamisi kwenda Moroni, Comoro, kurudiana na Komorozine katika Ligi ya Afrika. Picha na Mpigapicha Wetu
Muktasari:
Yanga inakwenda kurudiana na Wacomoro hao katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Awali Yanga ilishinda nyumbani mabao 7-0.
JESHI la wachezaji 19 la kikosi cha Yanga linaondoka leo Alhamisi alfajiri kuifuata Komorozine ya Comoro, lakini kocha mkuu wa timu hiyo, Hans Van Pluijm amewatema nyota kumi kwenye msafara wake wakiwamo kipa Juma Kaseja na mshambuliaji, Emmanuel Okwi.
Yanga inakwenda kurudiana na Wacomoro hao katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Awali Yanga ilishinda nyumbani mabao 7-0.
Kocha huyo alisema Kaseja aliyedaka kwenye mechi iliyopita, ameachwa kutokana na matatizo ya kiafya na Okwi ni kutokana na utata wa usajili wake.
“Bado tunataka ushindi, ukiangalia wachezaji ambao tunaondoka nao ni wale waliokuwa sawa katika mazoezi yetu ya wiki hii, hatutaki kwenda kujilinda sababu ya ushindi wetu wa mchezo wa kwanza,” alisema.
“Kuna uwezekano wa kikosi kitakachoshuka uwanjani siku ya Jumamosi kuwa na mabadiliko kidogo, lakini kwa sasa siwezi kukueleza nani na nani wataingia au kutoka, uamuzi wa mwisho tutafanya siku moja kabla ya mchezo.”
Licha ya Kaseja na Okwi, nyota wengine walioachwa ni viungo Nizar Khalfan, Salum Telela ambao ni wagonjwa kama ilivyo kwa washambuliaji Jerry Tegete, Reliants Lusajo, Shaaban Kondo na Hussein Javu pamoja na Bakari Masoud na beki Ibrahim Job.
Walioondoka ni makipa Deogratias Munishi ‘Dida’ na Ally Mustapha ‘Barthez’, Mabeki ni Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite na Rajab Zahir.
Viungo ni Athuman Idd ‘Chuji’, Frank Domayo, Haruna Niyonzima, Hassan Dilunga, Mrisho Ngassa, Simon Msuva, Hamis Thabitna David Luhende wakati washambuliaji ni Hamis Kiiza, Said Bahanuzi na Didier Kavumbagu.