Ziba Secondary yapiga mtu 14-0, sare zikitawala ligi ya wanawake

Muktasari:
- Ligi hiyo iliyoanza jana inashirikisha timu 19 na timu mbili zitapanda daraja la kwanza
Mwanza. BAADA ya kuanza kwa kichapo cha mabao 4-2 mbele ya Gets Program, leo mabingwa wa Tabora, Ziba Sekondari imezinduka na kushusha dozi nzito ikiichapa Ilula Queens mabao 14-0 katika mchezo wa raundi ya pili Ligi ya Mabingwa wa Mikoa kwa Wanawake (WRCL) inayoendelea jijini hapa.
Ziba Sekondari inayoundwa na wachezaji wanafunzi waliopatikana kwenye michezo ya Umisseta, imepata ushindi huo leo Julai 18, 2023 katika Uwanja wa Nyamagana, Mwanza mchezo ambao umepigwa kuanzia saa 8 mchana.
Timu hiyo imepata mabao hayo 14 kupitia kwa Mwatima Mwarabu aliyefunga mabao matano, Salma Mohamed na Hawa Haji waliofunga mabao manne kila mmoja na Rahima Hemed aliyetupia kambani bao moja.
Mwatima Mwarabu, Hawa Haji na Salma Mohamed wanaweka rekodi ya kuwa wachezaji wa kwanza kufunga mabao mengi katika mchezo mmoja kwenye michuano hiyo msimu huu tangu ilipoanza jana Jumatatu, ambapo Mwatima anafikisha mabao sita katika mechi mbili za timu yake baada ya jana kuifungia bao moja kwenye kichapo cha mabao 4-2 mbele ya Gets Program.
Kichapo hicho ni cha pili mfululizo kwa Ilula FDC ya Iringa ambayo mchezo wa kwanza ilichapwa mabao 6-1 na Raha Queens ya Simiyu, hivyo kujiweka njia panda katika safari ya kwenda nane bora licha ya kubakiza mechi mbili.
Katika mechi nyingine zilizopigwa leo katika Uwanja wa Nyamagana na Alliance, Mpaju Queens imeambulia sare ya 1-1 na Ifakara, huku Maendeleo Songwe na Kilimanjaro Wonders zikifungana mabao 2-2 na Raha Queens ikitoshana nguvu ya bao 1-1 na Young Star, wakati Singida Rising Star ikizinduka na kushinda mabao 3-2 mbele ya Mwanva FDC ya Shinyanga