Al-Hilal, Osimhen kuna jambo

Muktasari:
- Taarifa zinaeleza Osimhen ambaye awali aliweka wazi anataka kuendelea kucheza soka la kiushindani ameshafanya makubaliano binafsi na Al-Hilal ambayo inataka kumpa mshahara wa Pauni 29 milioni kwa mwaka.
RIYADH, SAUDI ARABIA: KWA mujibu wa mwandishi wa habari wa Italia, Sacha Tavolieri ni kamba straika wa Napoli na timu ya taifa ya Nigeria, Victor Osimhen yuko karibu zaidi kukamilisha uhamisho wake wa kudumu kwenda Al-Hilal ya Saudi Arabia.
Taarifa zinaeleza Osimhen ambaye awali aliweka wazi anataka kuendelea kucheza soka la kiushindani ameshafanya makubaliano binafsi na Al-Hilal ambayo inataka kumpa mshahara wa Pauni 29 milioni kwa mwaka.
Mbali ya kiasi hicho atakachopokea moja kwa moja kama mshahara, staa huyu pia atakuwa na bonasi mbalimbali kulingana na kiwango chake.
Al-Hilal wanapambana sana kufanikisha usajili wa staa huyu baada ya kufeli kumshawishi Bruno Fernandes ambaye ilimwekea zaidi ya Pauni 200 milioni kwa mkatabawa miaka mitatu.
Timu hii ambayo ndio bingwa mtetezi wa Ligi Kuu Saudi Arabia inataka kuboresha kikosi chao katika michuano ijayo ya Kombe la dunia la klabu litakaloanza mwezi huu huko Marekani.
Hata hivyo, licha ya makubaliano na mchezaji kufikiwa, Al-Hilal bado hawajafikia makubaliano na Napoli kuhusu ada ya uhamisho. Kwa mujibu wa mwandishi Gianluca Di Marzio, ofa yamwisho ambayo Al-Hilal imeiwasilisha kwa Napoli hadi sasa ni Euro 70 milioni, ambayo imekataliwa na Napoli imesisitiza inataka Euro 75 milioni.
Uhusiano wa Osimhen na Napoli siyo mzuri licha ya kusaini nao mkataba mpya katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi utakaomalizika mwaka 2026.
Hata hivyo, mkataba huo sasa unaingia mwaka wake wa mwisho, jambo linalowapunguzia nguvu Napoli kudai ada kubwa kwa mchezaji huyo wa kimataifa wa Nigeria, ambaye alifunga mabao 37 alipokuwa kwa mkopo Galatasaray msimu uliopita.
Mazungumzo kati ya timu hizo mbili juu ya ada ya uhamisho yanaendelea. Ikiwa Al-Hilal wataharakisha, wataweza kumtumia Osimhen katika Kombe la Dunia la Klabu la FIFA, ambalo lina dirisha maalumu la usajili linalomalizika Juni 10.