Amorim aanza mikakati ya usajili Man United

Muktasari:
- Inaelezwa Manchester United wako karibu kufikia makubaliano na mshambuliaji wa Wolves, Matheus Cunha, kwa ajili ya kumsajili katika dirisha lijalo.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim inadaiwa tayari ameshaingia chaka na kuanza kusuka upya kikosi chake na ameanza na safu ya ushambuliaji.
Inaelezwa Manchester United wako karibu kufikia makubaliano na mshambuliaji wa Wolves, Matheus Cunha, kwa ajili ya kumsajili katika dirisha lijalo.
Man United wanataka kutoa Pauni 62.5 milioni kama ada ya uhamisho lakini kwanza wanapambana kufikia makubaliano binafsi na wawakilishi wa staa huyu.
Tovuti ya Daily Mail, imeripoti kuwa Newcastle United wamekuwa wapinzani wakubwa kwa Man United katika dili hili na wanatamani kumsajili ili wakamtumie kama winga wa kushoto, lakini Cunha mwenyewe anaonekana kuvutiwa zaidi na Man United.
Ruben Amorim alionekana akizungumza na staa huyu mara baada ya kumalizika kwa mchezo wao dhidi ya Wolves uliopigwa kwenye uwanja Molineux, hali iliyozidi kuibua tetesi mambo yanaendelea vizuri.
Mbali ya Cunha ambaye anaweza kucheza zaidi ya nafasi moja, hivi karibuni mashetani hawa wekundu walidaiwa kuwa katika hatua nzuri ya kumsajili straika wa Nigeria, Victor Osimhen ambaye kwa sasa anacheza kwa mkopo Galatasaray.
Osimhen ambaye anaweza kucheza kama straika wa kati aliripotiwa ameshakubali kutua Man United na kinachosubiriwa ni mazungumzo baina ya timu hiyo na Napoli.
Straika mwingine ambaye yupo katika rada zao ni Liam Delap wa Ipswich Town lakini wanakumbana na ushindani mkali kutoka kwa Chelsea.
Mbali ya washambuliaji watakaoingia, pia kuna orodha ya mastaa wanaotarajiwa kuuzwa ili zipatikane pesa za kusajili ambao ni kama Marcus Rashford, Jadon Sancho, Antony, Casemiro, na Alejandro Garnacho.