Arsenal V PSG, London itasimama

Muktasari:
- Wakati wakitamba mitaani kwa shangwe, wapinzani walikuwa wakiwaangalia tu, ama kwa wivu au kuwapongeza. Hata hivyo, kwa vijana wa Mikel Arteta wao walikuwa zao bize wakijiandaa na jambo lao. Kuikaribisha Paris Saint Germain kwenye usiku wa Uefa.
LONDON, ENGLAND: ILIKUWA wikiendi murua kwa mashabiki wa Liverpool. Wikiendi ya kihistoria. Mataji 20 ya Ligi Kuu England, Jiji la Liverpool lilichafuka kwa shangwe, starehe, watu walikunywa, wakala na starehe za aina yote kufurahia ubingwa huo.
Wakati wakitamba mitaani kwa shangwe, wapinzani walikuwa wakiwaangalia tu, ama kwa wivu au kuwapongeza. Hata hivyo, kwa vijana wa Mikel Arteta wao walikuwa zao bize wakijiandaa na jambo lao. Kuikaribisha Paris Saint Germain kwenye usiku wa Uefa.
Ni mchezo wa kwanza wa hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Arsenal inaanzia nyumbani dhidi ya PSG mabingwa wa Ufaransa katika Uwanja wa Emirates, jijini London.

Arsenal baada ya kuona mambo kwenye Ligi Kuu Engalnd ni magumu sasa akili zao ni kwenye michuano hiyo migumu na mikubwa zaidi Ulaya na wanaona huko inawezekana.
Michuano hiyo ndiyo nafasi pekee kwa Arsenal msimu huu kufungua shampeni kwani hakuna kombe lingine la ubingwa wanaloweza kuchukua kwa kipindi hiki zaidi ya hilo.
Mchezo huu utakaopigwa kuanzia saa 4:00 usiku na utakuwa wa sita kwa timu hizi kukutana na Arsenal ndiyo inayonekana kuwa na rekodi nzuri zaidi na katika mechi tano, Arsenal imeshinda mbili na tatu zilizosalia zilimalizika kwa sare.

Timu hizi zimewahi kukutana katika hatua kama hii ya nusu fainali mwaka 1994 lakini ilikuwa ni kwenye michuano ya European Cup Winners' Cup na Arsenal ilipenya baada ya mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa Ufaransa kumalizika kwa sare kisha ikaenda kushinda England kwa bao 1-0, kisha washika mitutu hao wakaenda kuchukua ubingwa mbele ya Parma.
Mara ya mwisho kwa timu hizi kukutana katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ni mwaka jana hatua ya makundi na Arsenal ilishinda 2-0.
PSG ambayo imekuwa ikipambana sana kutafuta taji hili kwa muda mrefu, nao ni usiku wao muhimu ingawa bado watakuwa na faida ya uwanja wao wa nyumbani.
Matajiri hawa wa Jiji la Paris waliwahi kuvuka hatua kama hii mara moja mwaka 2020 na kucheza fainali ingawa walipoteza mbele ya Bayern Munich.

Kesho pia kutakuwa na nusu fainali ya pili kati ya Barcelona na Inter Milan itakayopigwa dimba la Estadi Olimpic Lluis Companys.
Mechi hii imebeba matumaini ya Barcelona ambayo inahitaji kushinda mataji matatu kwa mpigo msimu huu, baada ya kubeba Copa del Rey kwa kuichapa wapinzani wao Real Madrid mabao 3-2.
Barca na Inter zimekutana mara 12 katika michuano hii na Barcelona ndiyo ina rekodi nzuri zaidi ikishinda mara sita, sare nne na kufungwa mbili.
Mechi hii itakumbushia nusu fainali ya msimu wa 2009/10 na Inter ikiwa chini ya Jose Mourinho ilipita kwa tofauti ya mabao 4-1.
Mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa Italia ulimalizika kwa Inter kushinda 3-1 kisha marudiano Nou Camp ulimalizika kwa Barca kushinda bao 1-0. Mchezo huu pia utaanza saa 4:00 usiku.