Arteta akubali yaishe, ataka nafasi ya pili

Muktasari:
- Arsenal imeachwa pointi 15 na vinara Liverpool kwenye msimamo wa Ligi Kuu England baada ya kutibua mambo kwenye mbio za ubingwa, ikishindwa kupata ushindi kwenye mechi tatu za mwisho.
LONDON, ENGLAND: KOCHA Mikel Arteta amewataka mastaa wake wa Arsenal kushinda vita ya kumaliza namba mbili Ligi Kuu England msimu huu baada ya kuwaambia: “Kama hamuwezi kuwa namba moja, basi walau muwe namba mbili.”
Arsenal imeachwa pointi 15 na vinara Liverpool kwenye msimamo wa Ligi Kuu England baada ya kutibua mambo kwenye mbio za ubingwa, ikishindwa kupata ushindi kwenye mechi tatu za mwisho.
Chelsea inaweza kupunguza pengo la pointi kuikaribia Arsenal endapo kama itaibuka na ushindi katika mchezo wa ligi hiyo utakaofanyika uwanjani Emirates, Jumapili.
Arteta, ambaye kikosi chake kilimaliza nafasi ya pili kwa misimu miwili iliyopita, aliwaambia mastaa wake: “Wanachuana kuwania nafasi ya pili. Nadhani tangu kwenye kipindi cha pre-season na vile ninavyojua staili ya uchezaji ya Enzo na wachezaji aliokuwa nayo, kwa mtazamo wangu nilijua watakuwa washindani.
“Nadhani wanaweza kushindana na timu yoyote ile. Ni timu ngapi kwa sasa zinachuana kuwania nafasi ya pili? Nyingi. Bado kuna mechi nyingi. Bado kuna kupanda na kushuka na kuna mechi nyingi ngumu. Bado ni timu nyingi zinachuana.”
Alipoulizwa kwa nini kumaliza nafasi ya pili ni muhimu au kwa sababu inatoa tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, kocha Arteta alisema: “Ina maana. Napendelea kumaliza nafasi ya kwanza kuliko ya pili, ya pili kuliko ya tatu, ya tatu kuliko ya nne. Kama huwezi kuwa wa kwanza, basi kuwa wa pili. Ni hivyo.”
Arteta alisema mechi zilizobaki kwenye Ligi Kuu England msimu huu ni muhimu kwa ajili ya kukifanyia tathmini kikosi chake kinahitaji nini ili kiwe cha ushindani kwenye mbio za ubingwa msimu ujao.
“Tutatumia hii nafasi kutambua nini kimekosekana na tufanye nini kupiga hatua ya juu,” alisema.
Arsenal iliichapa Chelsea 5-0 kwenye mechi ya Emirates msimu uliopita, wakati mechi ya kwanza msimu huu iliishia 1-1.