Aston Villa ina jambo kwa De Bruyne

Muktasari:
- De Bruyne, mwenye umri wa miaka 33, alitangaza kupitia mitandao ya kijamii msimu huu utakuwa wa mwisho akiwa na Man City na ataondoka kama mchezaji huru Juni mwaka huu baada ya kuhudumu kwa miaka 10 Etihad.
BIRMINGHAM, ENGLAND: ASTON VILLA wamefanya mazungumzo ya ndani kuhusu uwezekano wa kumsajili nyota wa Manchester City anayetarajiwa kuondoka, Kevin De Bruyne, lakini huenda wakakumbana na ushindani mkubwa kutoka timu nyingine zinazomhitaji.
De Bruyne, mwenye umri wa miaka 33, alitangaza kupitia mitandao ya kijamii msimu huu utakuwa wa mwisho akiwa na Man City na ataondoka kama mchezaji huru Juni mwaka huu baada ya kuhudumu kwa miaka 10 Etihad.
Kwa mujibu wa Sky Sports, Villa wanapima uwezekano wa kumsajili kiungo huyo mahiri ili aendelee kucheza Ligi Kuu England.
Kiungo huyo wa kimataifa kutoka Ubelgiji hataki kuondoka England na kuihamisha familia yake kwani anaona itakuwa ni usumbufu, hivyo anahitaji kusaini na timu ya nchini humo, hali ambayo imeziweka timu nyingi kwenye foleni ya kumhitaji ikiwemo Villa ambayo imeshaanza mazungumzo na wawakilishi wake.
Hata hivyo, kikosi cha Unai Emery bado kitakumbana na ushindani mkali kuwania saini ya De Bruyne kwa sababu timu nne kutoka Ligi Kuu ya Marekani ikiwemo Inter Miami, Chicago Fire, NYCFC, na D.C. United tayari vimeonyesha nia ya kumhitaji, huku pia Como ya Italia ikihusishwa na mchezaji huyo wa zamani wa Wolfsburg.
Como ambayo inafundishwa na Cesc Fabregas, gwiji wa zamani wa Arsenal na Chelsea, inafikiria kumsajili kiungo huyo mshambuliaji majira ya kiangazi.
SunSport hapo awali ilifichua nyota wa Al-Nassr, Cristiano Ronaldo aliishauri timu yake impe De Bruyne ofa ambayo hawezi kukataa.
De Bruyne anachukuliwa kama mmoja wa viungo bora zaidi katika historia ya Ligi Kuu England baada ya kufunga mabao 107 na kutoa pasi za mabao 177 katika mechi 417 akiwa na Man City.
Nyota huyo wa zamani wa Genk pia ametwaa mataji sita ya Ligi Kuu England, Kombe la FA mara mbili, Kombe la Ligi mara tano na Ligi ya Mabingwa Ulaya mara moja ambayo iliwawezesha kuchukua mataji matatu kwa pamoja.
Lakini licha ya mafanikio hayo Etihad, imebainika uamuzi wa kutompa mkataba mpya ulifanywa na klabu, si mchezaji mwenyewe.
Baada ya ushindi wa mabao 2-0, De Bruyne alisema Mkurugenzi wa Soka Txiki Begiristain na Mkurugenzi Mtendaji Ferran Soriano walikutana naye kwa muda mfupi kumweleza mkataba wake hautaongezwa.