Bei ya tiketi Uefa ni balaa

Muktasari:
- Mechi ya fainali msimu huu itapigwa Mei 31 katika dimba la Allianz Arena, lakini ili uione uwanjani ni lazima ujipange maana viingilio vimepanda.
MUNICH, UJERUMANI: MASHABIKI wa soka wameliwakia Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) kwa kupandisha bei za tiketi za fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mechi ya fainali msimu huu itapigwa Mei 31 katika dimba la Allianz Arena, lakini ili uione uwanjani ni lazima ujipange maana viingilio vimepanda.
Mbali ya ongezeko la viingilio mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa, pia kumekuwa na ongezeko dogo la kila mwaka katika bei za tiketi za fainali za Europa League na Uefa Conference League.
Uuzaji wa tiketi za daraja la juu kwa fainali zote tatu za wanaume umeanza kupitia tovuti ya UEFA na utaendelea hadi Aprili 11.
Timu zitakazofika fainali zitatengewa viti 18,000 katika uwanja huo wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 64,500, huku 38,700 vikienda kwa mashabiki wengine wa timu tofauti.
Kwa kutumia sera ya Fans First (Mashabiki Kwanza), UEFA imetangaza kuwa wale wa timu zitakazofika fainali watapata tiketi kwa Pauni 60 (takriban Sh 206,798) ambazo zitazuiwa hadi timu zitakapopatikana.
Lakini mashabiki wa timu za fainali au wengine ambao timu zao hazitafika watatakiwa kulipa zaidi ikiwa wanataka kuwa katika majukwaa ya VIP ambapo bei zimepandishwa maradufu.
Bei za tiketi katika daraja la kwanza ambazo ni ghali zaidi zimepanda kwa asilimia 33 hadi Pauni 816 (Sh 2.8 milioni) kutoka Pauni 612 (Sh2.4 milioni).
Viti vya daraja la pili vinauzwa kwa Pauni 558 (Sh1.9 milioni) ambalo ni ongezeko la asilimia 30 kutoka Pauni 429 (Sh1.4 milioni) msimu uliopita.
Tiketi za daraja la tatu bei zimeshuka kidogo kutoka Pauni 160 (Sh551,461) hadi Pauni 154 (Sh530,781).
Na kama ilivyo kila fainali hoteli pia zinatarajiwa kuwa na ongezeko kubwa la bei ya malazi ya usiku mmoja, huku bei za ndege nazo zikitarajiwa kupanda.
Lakini watumiaji wa mitandao ya kijamii wamelaumu UEFA kwa upandishaji huo wa bei. Mmoja aliandika: “Inapaswa kuwa ni kuvunja sheria kutoza kiasi kikubwa kama hicho.”
Mwingine alisema: “Hii si sawa. Hii ni akili ya kichaa, ni ngumu sana kumudu.”