Conor Gallagher hashikiki Atletico

Muktasari:
- Gallagher, 24, alikuwa kwenye kikosi cha The Blues tangu akiwa ana umri wa miaka sita na aliachana na timu hiyo badaa ya miaka 18, alipokwenda kujiunga na Atletico Madrid kwa ada ya Pauni 34 milioni kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi.
MADRID, HISPANIA: KIUNGO, Conor Gallagher ameendelea kuwasha moto huko Atletico Madrid alikojiunga akitokea Chelsea baada ya kucheza kwa kiwango cha mchezaji bora wa mechi kwenye mikikimikiki ya La Liga.
Gallagher, 24, alikuwa kwenye kikosi cha The Blues tangu akiwa ana umri wa miaka sita na aliachana na timu hiyo badaa ya miaka 18, alipokwenda kujiunga na Atletico Madrid kwa ada ya Pauni 34 milioni kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Na sasa maisha yake yanakwenda vizuri kwelikweli huko Hispania, ambako alitamba na miamba hiyo ya Wanda Metropolitano baada ya kukifungia kikosi cha Diego Simeone kwenye ushindi wa 3-0 dhidi ya Valencia.
Mwingereza huyo alionyesha kiwango bora kabisa kwenye mechi nyingine ya La Liga juzi Jumapili huko Rayo Vallecano, ambapo alifunga bao la kusawazisha kwenye sare ya 1-1. Alexander Sorloth aliambaa na mpira na kuingia kwenye eneo la Rayo kabla ya kumpasia Gallagher, ambaye alipiga shuti na kumshinda kipa Augusto Batalla.
Mashabiki wamekoshwa na kiwango cha staa huyo aliyewahi pia kucheza kwa mkopo Crystal Palace, huku wengine wakiamini kocha Simeone amefanya kazi ya ziada kumfanya kiungo huyo kuwa moto uwanjani na kufiti kwa staili yake akiwa bora tofauti na alivyokuwa Chelsea.
Shabiki mmoja alisema: “Conor Gallagher ni aina ya mchezaji wa Diego Simeone, Chelsea wamemtupa.”