Duh! Amorim hafiki Krismasi

Muktasari:
- Man United, waliendeleza msururu wa matokeo mabovu wikiendi iliyopita baada ya kulazimisha sare ya dakika za 'jiooni' dhidi ya Bournemouth.
MANCHESTER, ENGLAND: KIUNGO wa zamani wa Tottenham, Jamie O'Hara amesema haoni kama kocha wa Manchester United, Ruben Amorim ataendelea kusalia kwenye timu baada ya Krismasi ya mwaka huu.
Man United, waliendeleza msururu wa matokeo mabovu wikiendi iliyopita baada ya kulazimisha sare ya dakika za 'jiooni' dhidi ya Bournemouth.
Mashetani Wekundu wamegeuzia akili zao katika michuano ya Europa League ambako wapo hatua ya nusu fainali na wanapambana kushinda taji huko ili kufuzu ushiriki wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Msimu huu Man United imeweka rekodi ya kuwa msimu wao mbaya zaidi katika historia yao hata kama watafanikiwa kushinda mechi zao tano zilizosalia.
Akizungumza na Grosvenor Sport, O'Hara alisema: "Ruben Amorim atakuwa kwenye hatari ya kuondoka Manchester United kabla ya Krismasi. Hawawezi kuendelea hivi. Hata kama watashinda Europa League, hali yao ya ligi haijakuwa bora vya kutosha.
"Kabla ya kuzungumzia matatizo yao makubwa ya uwanjani na nje ya uwanja, sioni timu inaenda wapi, haieleweki wanataka mafanikio gani, wachezaji ambao Amorim anao hawatoshi kucheza katika mfumo ambao yeye anauhitaji, kuna wakati wameonekana kucheza vizuri, lakini ukitafuta wachezaji ambao anaweza kuwategemea labda ni Bruno Fernandes pekee."