Vigogo wapigana vikumbo kwa Jonathan David

Muktasari:
- David ambaye tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 46 za michuano yote, amefunga mabao mabao 25 na kutoa asisti 11.
NEWCASTLE United, Manchester United, Tottenham, West Ham, Chelsea, na Liverpool zimeonyesha nia ya kumsajili mshambuliaji wa Lille na timu ya taifa ya Canada, Jonathan David, 25, dirisha lijalo la majira ya kiangazi pale mkataba wake utakapomalizika.
Wakati huo huo, mabosi wa Lille pia wamempa ofa ya kusaini mkataba mpya wa kuendelea kusalia kwenye kikosi chao lakini staa huyu amegoma na kusisitiza anahitaji kuondoka.
David ambaye tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 46 za michuano yote, amefunga mabao mabao 25 na kutoa asisti 11.
Timu nyingi zimevutiwa sana na zinataka kumsajili fundi huyu kutokana na uwezo wake wa kutoa asisti na kufunga.
Cristian Romero
ATLETICO Madrid wamemweka beki wa Tottenham na timu ya taifa ya Argentina, Cristian Romero, mwenye umri wa miaka 27, katika orodha ya mastaa ambao inayohitaji sana kuwasajili dirisha lijalo la majira ya kiangazi mwaka huu. Romero ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, msimu huu akiwa na Atletico amecheza mechi 23 za michuano yote.
Matheus Cunha
MANCHESTER United imempa ofa ya mkataba wa miaka mitano, mshambuliaji wa Wolves na timu ya taifa ya Ureno, Matheus Cunha ikiwa ni ofa yao ya kutaka kumsajili dirisha hili. Cunha mwenye umri wa miaka 25, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2029. Msimu huu amecheza mechi 32 za michuano yote na kufunga mabao 17.
Kenan Yildiz
CHELSEA inajitahidi sana kutaka kumsajili mshambuliaji wa Juventus na timu ya taifa ya Uturuki, Kenan Yildiz, mwenye umri wa miaka 19, lakini wanakutana na ushindani wa kutosha kutoka kwa Arsenal, Liverpool, Manchester United na Manchester City ambazo pia zinahitaji huduma ya staa huyu. Yildiz ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2029, msimu huu amecheza mechi 46 za michuano yote na kufunga mabao manane.
Liam Delap
MANCHESTER United bado wana nia ya kumsajili mshambuliaji wa Crystal Palace, Mfaransa Jean-Philippe Mateta, mwenye umri wa miaka 27, ikiwa hawatofanikisha kumsajili mshambuliaji wa Ipswich Town, Liam Delap, mwenye umri wa miaka 22. Delap ambaye yupo katika rada za timu nyingi kubwa barani Ulaya, msimu huu amefunga mabao 12.
Kim Min-jae
NEWCASTLE United wako katika mazungumzo ya kumsajili beki wa kimataifa wa Korea Kusini, Kim Min-jae, mwenye umri wa miaka 28, kutoka Bayern Munich dirisha hili la majira ya kiangazi. Mabosi wa Newcastle wanaamini staa huyu atasaidia sana eneo lao la ulinzi ikiwa watampata. Mbali ya Kim, Newcastle pia inawawinda mabeki wengine ambao ni pamoja na Ousmane Diomande (21), Malick Thiaw(23), Jan Paul van Hecke (24).
Mohammed Kudus
WINGA wa West Ham na timu ya taifa ya Ghana, Mohammed Kudus mwenye umri wa miaka 24, ameingia katika rada za Al-Nassr inayoshiriki Ligi Kuu ya Saudi Arabia ambayo ipo tayari kumsajili dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Kudus anaonekana kuwa ingizo sahihi kwenye safu ya ushambuliaji ya AL Nassr kutokana na kiwango bora ambacho amekuwa akikionyesha tangu atue West Ham.
Dejan Kulusevski
TOTTENHAM imeanza mazungumzo na wakala wa kiungo wao raia wa Sweden, Dejan Kulusevski, 24, ili kumsainisha mkataba mpya na kumzuia asiondoke dirisha lijalo la majira ya kiangazi na vigogo kibao wameonyesha nia ya kumsajili zikiwamo AC Milan na Napoli.
Kocha wa Spurs, Ange Postecoglu bado ana mipango na Dejan na hataki kuona akiondoka. Mkataba wake unamalizika mwaka 2028.