Garnacho, Mainoo bado wapo sokoni Man United

Muktasari:
- Garnacho na Mainoo wanadaiwa kuwa hawamfurahishi kocha Ruben Amorim katika uchezaji wao.
MANCHESTER United bado ina mpango wa kuwauza mastaa wake wawili - winga raia wa Argentina, Alejandro Garnacho, 20, na kiungo kutoka England, Kobbie Mainoo, 19, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Garnacho na Mainoo wanadaiwa kuwa hawamfurahishi kocha Ruben Amorim katika uchezaji wao.
Katika dirisha lililopita Napoli na Chelsea ni miongoni mwa timu zilizokuwa zinahitaji saini za wachezaji hao, lakini mchakato ulichelewa kukamilika na moja kati ya sababu zilizochangia ni kiasi kikubwa cha pesa kilichotakiwa na Man United.
Garnacho aliyehusishwa na Napoli, Man United ilikuwa inataka Pauni 70 milioni, wakati Chelsea iliyomtaka Mainoo ilitakiwa kutoa Pauni 80 milioni. Mkataba wa sasa wa Mainoo unamalizika 2027 ilhali ule wa Garnacho unatarajiwa kumalizika 2028.
KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta bado anaitaka saini ya straika wa Juventus na Serbia, Dusan Vlahovic, 24,ambaye alihitaji asajiliwe dirisha lililopita la majira ya kiangazi, lakini ilishindikana. Vlahovic alikuwa katika orodha ya mastaa waliopendekezwa na Arteta kusajiliwa ili kuboresha safu yake ya ushambuliaji. Dili hilo linadaiwa kukwama kutokana na masuala ya kifedha.
KIUNGO wa Southampton, Tyler Dibling ambaye alihusishwa na Tottenham Hotspur pamoja na RB Leipzig katika dirisha lililopita, inadaiwa alikataa mwenyewe kuondoka katikati ya msimu na badala yake atafanya hivyo msimu utakapomalizika. Tyler amezivutia timu nyingi kutokana na kiwango bora alichoonyesha tangu kuanza kwa msimu huu. Timu zote zilikuwa tayari kutoa zaidi ya Pauni 20 milioni kwa ajili ya kufanikisha mchakato wa kumsajili.
ATALANTA itakuwa tayari kumwachia staa raia wa Nigeria, Ademola Lookman, 27, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi baada ya kumzuia kuondoka dirisha lililopita. Lookman ambaye anahusishwa na timu mbalimbali za England, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2026. Msimu huu amecheza mechi 26 za mic.huano yote na kufunga mabao 14.
FENERBAHCE bado ina mpango wa kumsajili winga wa Barcelona na Hispania, Ansu Fati, 22, katika dirisha hili kwa mkopo, ambapo Uturuki bado halijafungwa. Fati alitajwa katika orodha ya kuondoka Barca dirisha lililopita ili kuiwezesha timu hiyo kufanya usajiliwa mastaa wengine. Dirisha la usajili la Uturuki kwa majira ya baridi linatarajiwa kufungwa Februari 11.
MSHAMBULIAJI wa Wolves na Brazil, Matheus Cunha, 25, bado anatamani kuondoka kwenye timu hiyo katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi licha ya kusaini mkataba mpya ambao unaomalizika 2029. Cunha mwenye umri wa miaka 25, ni miongoni mwa mastaa tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Wolves na msimu huu amecheza mechi 24 za michuano yote na kufunga mabao 11.
INAELEZWA mabosi wa Nottingham Forest walikataa ofa kubwa kutoka Chelsea katika dakika za mwisho za diirisha lililopita la majira ya baridi kwa ajili ya beki raia wa Brazil, Murillo, 22. Ofa hiyo nono iliyowekwa mezani na Chelsea inadaiwa kuwa ingemfanya Murillo mchezaji aliyeuzwa kwa beki kubwa zaidi katika historia ya Nottingham.
MANCHESTER City inataka kurudi tena mezani ili kufanya mazungumzo na Juventus kuipata saini ya beki kisiki wa timu hiyo na Italia, Andrea Cambiaso, 24, katika dirisha la majira ya kiangazi. Cambiaso ambaye ni mmoja kati ya wachezaji tegemeo wa kikosi cha kwanza cha Juventus alihitajiwa Man City tangu dirisha lililopita.