Greenwood hali si shwari

Muktasari:
- Greenwood, mwenye umri wa miaka 23, amekuwa hapati nafasi ya kutosha baada ya kocha De Zerbi kufunguka kwamba staa huyo hajitumi.
MARSEILLE, UFARANSA: MSHAMBULIAJI wa Marseille, Mason Greenwood huenda akaondoka katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi baada ya kocha Roberto de Zerbi kuendelea kutofurahishwa na utendaji kazi wake.
Greenwood, mwenye umri wa miaka 23, amekuwa hapati nafasi ya kutosha baada ya kocha De Zerbi kufunguka kwamba staa huyo hajitumi.
Mshambuliaji huyo, aliyejiunga na Marseille akitokea Manchester United katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana, alikuwa mchezaji wa kudumu katika kikosi cha Marseille tangu atue, lakini hivi karibuni hapati nafasi ya kucheza na alikuwa benchini katika mechi dhidi ya Lens na PSG katika wiki za hivi karibuni.
Kocha De Zerbi alisema ni lazima staa huyo abadilike kama anataka kuendelea kupata nafasi katika timu.
Kocha huyo wa zamani wa Brighton alisema: "Hakuna ambaye ana heshima zaidi kwake kuliko mimi.
"Lakini hiyo haiathiri chochote: Natarajia zaidi kutoka kwake. Lazima afanye zaidi, kwa sababu kile anachoonyesha sasa hakitoshi.
"Kama anataka kufikia lengo lake la kuwa mchezaji bora, lazima aonyeshe shauku na utendaji kazi zaidi."
Greenwood bado anaendelea kuwa mchezaji wa pili kufunga mabao mengi katika Ligue 1 msimu huu ikiwa ni msimu wake wa kwanza.
Hata hivyo, mtangazaji wa RMC Florent Germain, kupitia BFM Marseille, alieleza kuwa ikiwa Greenwood, ambaye aliwahi kuwa mchezaji wa kimataifa wa England, hatamridhisha De Zerbi, hadi mwisho wa msimu huu, kuna uwezekano mkubwa akauzwa.
"Ni mchezaji ambaye anaweza kuleta tofauti kubwa katika timu kutokana na uwezo wake, lakini ikiwa hatafikia kufanya vile ambavyo kocha anahitaji, atauzwa tu."
Greenwood alihusishwa na timu nyingi tofauti katika dirisha lililopita ikiwamo Barcelona, PSG na Juventus lakini zilishindwa kumpata.
Staa huyu alicheza kwa mkopo Getafe kwa msimu uliopita na kiwango chake kilisababisha timu nyingi kutamani kumsajili.
Ikiwa atauzwa, Man United itapata faida kwa kukunja asilimia 50 ya mauzo yake kama sehemu ya vipengele vilivyowekwa katika mkataba wa mauziano kati yao na Marseille.