Gyokeres haifikirii kabisa Man United

Muktasari:
- Man United imeripotiwa kuwa kwenye msako wa straika mpya na Kocha Ruben Amorim amekuwa akihusishwa na Gyokeres, 26, mchezaji ambaye alimnoa walipokuwa pamoja Sporting CP.
LISBON, URENO: KLABU saba ambazo straika Viktor Gyokeres amefungua milango ya kwenda kujiunga nazo dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi zimewekwa bayana na Manchester United hawamo kwenye orodha.
Man United imeripotiwa kuwa kwenye msako wa straika mpya na Kocha Ruben Amorim amekuwa akihusishwa na Gyokeres, 26, mchezaji ambaye alimnoa walipokuwa pamoja Sporting CP.
Amorim alimnunua straika huyo wa Sweden kwa ada ya Euro 20 milioni mwaka 2023 na alikwenda kufunga mabao 66 katika mechi 68 kabla ya kocha huyo Mreno kujiunga na Man United.
Straika ameendelea kuwasha moto hata baada ya kocha Amorim kuondoka huko Sporting CP na sasa amekuwa mmoja wa mastraika wanaosakwa kwa udu na uvumba huko Ulaya.
Man United, Arsenal na Chelsea zote zimekuwa zikihusishwa na mshambuliaji huyo kwa upande wa Ligi Kuu England, lakini Barcelona na Paris Saint-Germain nazo zimetajwa. Lakini, sasa timu ambazo staa huyo wa zamani wa Coventry City anazifikiria kwenda zimeshafahamika.
Gazeti la A Bola ya Ureno limefichua ishu ya kwenda Man United au Chelsea haupo kwenye mpango wa Gyokeres na badala yake, straika huyo mwenye umri wa miaka 26, amefungua milango ya kwenda Arsenal, Liverpool, Manchester City, Real Madrid, Barcelona, PSG au Bayern Munich.
Gyokeres kwa sasa bado ana mkataba Sporting hadi 2028. Na miamba hiyo Ureno iligomea ofa ya kumpiga bei mshambuliaji huyo dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana na kuweka kipengele kwenye mkataba huo, ikitaja bei anayoweza kuuzwa mkali huyo ni Euro 100 milioni (Pauni 84 milioni).
Rais wa Sporting, Frederico Varandas alisema Novemba mwaka jana hawatakuwa na nguvu ya kumzuia straika huyo asiondoke kama kuna timu itakayokuwa tayari kulipa kiwango hicho kilichowekwa kwenye mkataba.
“Siwezi kuahidi chochote,” alisema Varandas.
“Kama kuna klabu itakuja na kulipa kiasi hicho cha pesa na mwenyewe kama atataka kuondoka, ataondoka.”
Sasa straika Gyokeres mwenyewe amegoma kufuta uwezekano wa kuachana na timu hiyo dirisha lijalo la majira ya kiangazi baada ya kusema anasubiri kuona kitakachotokea.