Hansi Flick kubadili falsafa Barcelona

Muktasari:
- Jumamosi iliyopita, walishinda 1-0 dhidi ya Leganes, bao pekee likitokana na kujifunga kwa Jorge Saenz, pia beki wao Inigo Martinez aliokoa bao la kusawazisha katika dakika za mwisho.
BARCELONA, HISPANIA: KOCHA wa Barcelona, Hansi Flick anaonekana kubadilisha falsafa ya timu hiyo kutoka kumiliki mpira muda wote hadi kupenda kujilinda zaidi baada ya yeye mwenyewe kukiri safu yake ya ulinzi ndio itakayomwezesha kushinda taji badala ya safu yake ya kiungo na ushambuliaji kwa jumla.
Barcelona wamekuwa wakifunga mabao mengi msimu huu, hadi sasa wakiwa wamefunga mabao 127 katika mashindano yote.
Jumamosi iliyopita, walishinda 1-0 dhidi ya Leganes, bao pekee likitokana na kujifunga kwa Jorge Saenz, pia beki wao Inigo Martinez aliokoa bao la kusawazisha katika dakika za mwisho.
Safu ya ulinzi ya Barcelona imekuwa bora msimu huu ikisaidiwa zaidi na safu yao ya ushambuliaji ambayo imekuwa ikikaba kuanzia juu na tangu mwanzoni mwa mwaka huu, Barca ndio timu iliyoruhusu mabao machache zaidi kuliko Inter Milan na Atletico Madrid, ambazo zinajulikana kwa safu zao za ulinzi madhubuti.
Flick amesema safu ya ulinzi ndiyo itakayokuwa silaha yao kuu katika kipindi kilichosalia cha msimu huu wanaopambana kushinda mataji matatu.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya ushindi dhidi ya Leganes, Flick alisema:
“Ilikuwa mechi ngumu na muhimu sana kwetu. Najivunia kile ambacho timu yangu imefanya katika wiki na miezi iliyopita. Kitu kinachojitokeza zaidi ni kujitolea kwa wachezaji. Najivunia sana timu yangu inavyokaba.”
Flick huenda akafanya mabadiliko katika kikosi chake kwa mechi ijayo ya mkondo wa pili wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Borussia Dortmund, baada ya mchezo wa mkondo wa kwanza kushinda 4-0.