Hawa hapa Makipa wanaomnyima usingizi Amorim

Muktasari:
- Kipa namba mbili raia wa Uturuki, Altay Beindir alisimama langoni dhidi ya Newcastle United lakini mambo yaliendelea kuwa magumu baada ya kuruhusu mabao manne na Man United kupoteza mchezo kwa mabao 4-1 kwenye Uwanja wa St. James' Park.
MANCHESTER, ENGLAND: JUMAPILI iliyopita, Kocha wa Manchester United, Ruben Amorim alimpumzisha kipa wake, Andre Onana baada ya kufanya makosa yaliyoigharimu kwenye mechi ya robo fainali ya Europa League dhidi ya Lyon ya Ufaransa.
Kipa namba mbili raia wa Uturuki, Altay Beindir alisimama langoni dhidi ya Newcastle United lakini mambo yaliendelea kuwa magumu baada ya kuruhusu mabao manne na Man United kupoteza mchezo kwa mabao 4-1 kwenye Uwanja wa St. James' Park.
Ripoti zinaeleza, Amorim hana imani na makipa alionao kwa sasa na tayari amewasilisha majina ya makipa watano kwa mabosi wa timu hiyo akitaka wasajiliwe ifikapo mwisho wa msimu huu. Hawa hapa.

Bart Verbruggen
Inadaiwa Mashetani Wekundu waliwasiliana na Brighton kuulizia upatikanaji wa Mholanzi huyo.
Verbruggen, mwenye umri wa miaka 22, amekuwa na kiwango cha kuvutia tangu ajiunge na Brighton kwa Pauni 16 milioni mwaka 2023 licha ya kwamba ana clean sheets sita pekee msimu huu wa Ligi Kuu.
Bart ameshachezea timu ya taifa ya Uholanzi mechi 20, na kiwango chake mbali ya Man United pia kimevutia Bayern Munich wanaoweza kushindana na Man United kumsajili kipa huyo dirisha lijalo. Brighton inadaiwa kuhitaji Pauni 60 milioni ili kumuuza.

Zion Suzuki
Kipa huyu raia wa Japan ameendelea kuhusishwa na uhamisho kwenda Old Trafford madirisha kadhaa yaliyopita ya usajili.
Man nited ilituma maskauti wake kumtazama mwaka jana lakini wakachelewa na Parma ikaibuka katikati ya kumsajili.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 hajafanya kosa lolote lililosababisha bao katika Serie A na sasa thamani yake imepanda hadi Paun 40 milioni kiasi ambacho Parm inakihitaji ili kumuuza baada ya wao kumnunua kwa Pauni 6.5 milioni tu.

Lucas Chevalier
Chevalier amezivutia timu nyingi kutokana na kiwango chake akiwa na Lille katika Ligue 1 na Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.
Yupo kwenye rada ya Manchester United na Manchester City huku ripoti zikidai Paris Saint-Germain na AC Milan wanaweza kujaribu kuingilia dili hilo.
Mfaransa huyo, mwenye umri wa miaka 23, ana mkataba na Lille hadi mwaka 2027 lakini anaweza kuuzwa kwa Pauni 40 milioni. Chevalier ametajwa kuwa mrithi wa kipa namba moja wa Ufaransa Mike Maignan

Diogo Costa
Costa ni kipa mwingine ambaye amekuwa akihusishwa mara kwa mara na Man United.
Kipa huyu namba moja wa Porto ana uwezo mkubwa wa kucheza akiwa na mpira mguuni pia kuokoa mashuti makali na hapo awali aliwahi kusema angependa kuichezea Man United.
Costa, mwenye umri wa miaka 25, alisema: "Kwangu mimi, wao(Man United) ni timu kubwa zaidi England, klabu maalum ambayo nimekuwa nikiipenda tangu utotoni.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ureno ana kipengele cha kuachiliwa kwa Pauni 62.5 milioni.

Senne Lammens
Ingawa sio maarufu, Lammens ni kipa mwingine ambaye ameonekana kutazamwa kwa jicho ka tatu na Man United.
Hadi sasa staa huyu amecheza mechi 51 tu za kimashindano akiwa na Royal Antwerp na aliitwa kwa mara ya kwanza katika kikosi cha timu ya taifa ya Ubelgiji Machi mwaka huu.
Man United tayari imetuma wawakilishi wake kwenda kumtazama kijana huyo mwenye umri wa miaka 22, ambaye inasemekana anaweza kuuzwa kwa Pauni 30 milioni.