Hebu sikieni Mbappe kuna kitu kasema

Muktasari:
- Miamba hiyo ya Hispania ilijikuta ikichapwa 3-0 na Arsenal katika mchezo wa kwanza wa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya uwanjani Emirates.
MADRID, HISPANIA: SUPASTAA, straika Kylian Mbappe amewaambia wachezaji wenzake wa Real Madrid wanapaswa kujitazama baada ya kiwango cha hovyo walichokionyesha kwenye mechi dhidi ya Arsenal usiku wa Jumanne.
Miamba hiyo ya Hispania ilijikuta ikichapwa 3-0 na Arsenal katika mchezo wa kwanza wa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya uwanjani Emirates.
Mabao mawili ya Declan Rice na moja la Mikel Merino yalitosha kuifanya Arsenal ya kocha Mikel Arteta kujiweka kwenye wakati mzuri wa kusonga mbele, lakini Mbappe ametoa ujumbe mwepesi tu kwa wenzake kuelekea mechi ijayo.
Akitumia ukurasa wake wa Instagram, fowadi huyo Mfaransa alituma picha yake ya kwenye mechi hiyo na kuweka maneno haya: “Hay que creer hasta el final” yakiwa na maana “yakupasa kuamini hadi mwisho kabisa.”
Mbappe, 26, alikuwa na maana kwamba anaamini bado kuna kitu kinaweza kufanyika kwenye mechi ya marudiano itakayofanyika uwanjani Bernabeu wiki ijayo. Straika huyo tayari ameshafunga mabao 32 msimu huu, ambao ni wa kwanza kwake kwenye kikosi hicho cha miamba ya Hispania.
Na yeye si mchezaji pekee wa Real Madrid ambaye hajakata tamaa kwamba timu yao imetoka wakati kuna mechi ya pili itakayotoa uamuzi wa mwisho. Kiungo Mwingereza, Jude Bellingham anaamini watakwenda kupindua meza kwenye mechi hiyo ijayo na kufuta kiwango chao cha hovyo walichokionyesha uwanjani Emirates.
"Hatukuwa kwenye ubora wetu kabisa," alisema Bellingham.
"Huo ndio ukweli na Arsenal walikuwa wazuri sana. Najua mabao yao mawili ni ya friikiki, lakini walikuwa vizuri. Kuna mechi ya marudiano na hiyo ndiyo tuliyobakiza. Tunahitaji kufanya kitu spesho, kitu cha kushangaza na sehemu moja ya vitu kama hivyo ni nyumbani kwetu.
"Tuna dakika 90 zaidi za kucheza nyumbani na kufanya kitu. Bado hatujafa, tuna dakika 90 kwenye soka na chochote kinaweza kutokea Bernabeu."
Kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti alisema kupindua meza kunahitaji ujanja mwingi huku akisema: "Matokeo yanaonyesha Arsenal walikuwa vizuri zaidi yetu. Mechi ilikuwa tofauti sana. Kwa dakika 60 tulikuwa sare, kisha wakafunga kwa friikiki mbili matata. Mechi ikabadilika."