Inter Miami yajisogeza kwa Kevin de Bruyne

Muktasari:
- De Bruyne ambaye ataondoka Man City mwisho wa msimu kama mchezaji huru baada ya mkataba wake kumalizika, ameweka wazi kuwa hadi sasa bado hajaamua wapi atakwenda ingawa bado anatamani kuendelea kucheza soka la kiushindani.
INTER Miami inatamani sana kumsajili kiungo wa Manchester City na timu ya taifa ya Ubelgiji, Kevin de Bruyne, 33, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
De Bruyne ambaye ataondoka Man City mwisho wa msimu kama mchezaji huru baada ya mkataba wake kumalizika, ameweka wazi kuwa hadi sasa bado hajaamua wapi atakwenda ingawa bado anatamani kuendelea kucheza soka la kiushindani.
Licha ya matamanio ya huduma yake, ripoti zinaeleza kwamba mazungumzo baina ya wawakilishi wa kiungo huyu na Inter Miami bado hayajafikia sehemu nzuri.
Kumekuwa na tetesi zinazomhusisha De Bruyne na timu za Saudi Arabia lakini hadi sasa bado hakuna ofa yoyote rasmi iliyotumwa kwa mawakala wa staa huyu.
De Bruyne anaondoka Man City ikiwa ni baada ya kuhudumu kwa miaka 10 katika kikosi hicho cha kocha Pep Guardiola.
Felix Nmecha
MANCHESTER United inapambana kumsajili kiungo wa Borussia Dortmund na timu ya taifa ya Ujerumani, Felix Nmecha, 24, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ambapo watatakiwa kulipa Pauni 40 milioni ili kufanikisha mchakato huo.
Nmecha ni miongoni mwa wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Dortmund na msimu huu amecheza mechi 30 za michuano yote.
Xavi Simons
LIVERPOOL bado ina mpango wa kumsajili kiungo wa RB Leipzig na timu ya taifa ya Uholanzi, Xavi Simons, 21, ambaye atapatikana kwa Euro 80 milioni ifikapo dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Simons ambaye alisaini mkataba wa kudumu na Leipzig katika dirisha lililopita la majira ya kiangazo baada ya kuitumikia kwa mkopo wa msimu mmoja, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
Kepa Arrizabalaga
BOURNEMOUTH inataka kumsainisha mkataba wa kudumu kipa wake raia wa Hispania, Kepa Arrizabalaga, 30, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi lakini pia bado wanahitaji saini ya kipa wa Liverpool na Jamhuri ya Ireland, Caoimhin Kelleher, ambaye ameomba kuandoka katika kikosi cha majogoo kwa sababu hapati nafasi ya kutosha.
Jarrel Hato
ARSENAL , Liverpool na Chelsea zote zimeandaa mkwanja wa kutosha kwa ajili ya kumsajili beki kisiki wa Ajax na timu ya taifa ya Uholanzi, Jarrel Hato, 19, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Licha ya nia yao ya kutaka kumsajili staa huyu ameonyesha matamanio ya kutua Real Madrid ambayo pia imeanza mazungumzo na wawakilishi wake.
Darwin Nunez
LIVERPOOL inataka kutumia karibia Pauni 100 milioni katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka huu ili kusajili straika mpya baada ya kumuweka sokoni staa wao Darwin Nunez.
Inaelezwa kocha Arne Slot havutiwi sana na kiwango cha Nunez hivyo ameruhusu aondoke.
Mkataba wa staa huyu wa Uruguay unamalizika mwaka 2028.
Luis Diaz
AL NASSR ya Saudi Arabia imetua kwa winga wa Liverpool na timu ya taifa ya Colombia, Luis Diaz ambaye imepanga kumsajili katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi baada ya kuona uwezekano wa kuipata huduma ya mshambuliaji wa Real Madrid na timu ya taifa ya Brazil, Vinicius Junior inakuwa changamoto.
Tangu mwaka jana Diaz amekuwa akihusishwa na Barcelona ambayo ni ndoto yake kujiunga nayo.
Liam Delap
EVERTON imeungana na timu nyingine za EPL katika harakati za kutaka kumsajili straika wa Ipswich Town na timu ya taifa ya England kwa vijana wenye umri chini ya miaka 21, Liam Delap, 22, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Delap ni mmoja kati ya mastraika walioonyesha kiwango bora kwa msimu huu ambapo amefunga mabao 12 katika mechi 34.