Iran hatarini kukosa Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- Ili kutatua mkwamo huo, viongozi wa soka wa Iran wanatarajia kufanya mkutano wa dharura na usimamizi wa FIFA ili kupata dhamana ya kusafiri, huku wachezaji wakipangiwa kwenda nchini Uturuki kwa ajili ya kukamilisha taratibu za utambulisho wa alama za vidole.
Mkuu wa Shirikisho la Soka la Iran, Mehdi Taj, ametangaza kuwa hadi sasa hakuna kibali cha kuingia nchini Marekani (visa) hata kimoja kilichotolewa na serikali ya nchi hiyo kwa ajili ya timu ya taifa kuelekea Fainali za Kombe la Dunia 2026.
Hatua hii inaleta sintofahamu kubwa baada ya kikosi hicho kufanyiwa sherehe rasmi ya kuagwa mjini Tehran.
Ili kutatua mkwamo huo, viongozi wa soka wa Iran wanatarajia kufanya mkutano wa dharura na usimamizi wa FIFA ili kupata dhamana ya kusafiri, huku wachezaji wakipangiwa kwenda nchini Uturuki kwa ajili ya kukamilisha taratibu za utambulisho wa alama za vidole.
Kutokana na mkwamo huo wa kidiplomasia, ratiba ya maandalizi ya timu hiyo iliyopewa jina la "Team Melli" ipo hatarini kuvurugika.
Kikosi hicho kilitarajiwa kuwasili nchini Marekani mapema mwishoni mwa mwezi Mei, mara baada ya kumaliza kambi yao ya mazoezi nchini Uturuki na kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Gambia.
Walikuwa wamepanga kuweka kambi yao kuu ya mashindano mjini Tucson, Arizona, ili kuzoea mazingira kabla ya ufunguzi rasmi wa mashindano hayo makubwa duniani Juni 11, 2026.
Katika droo ya makundi ya Kombe la Dunia 2026, Iran imepangwa Kundi G linalojumuisha pia timu za Ubelgiji, Misri na New Zealand.
Mechi ya kwanza ya Iran imepangwa kupigwa Juni 15, 2026, ambapo itachuana na New Zealand katika uwanja wa SoFi uliopo Los Angeles, California. Wadau wengi wa soka ulimwenguni sasa wanasubiri kuona kama FIFA itafanikiwa kuishawishi Marekani kutoa vibali hivyo ili kuepusha kashfa ya kisiasa michezoni.