Kigari cha kubeba majeruhi uwanjani chagonga mchezaji
Muktasari:
- El Nacional na Liga de Portoviejo zilikuwa zikimenyana katika mchezo wa ligi hiyo, ambapo wageni (Portoviejo) walishinda kwa bao 1-0. Hata hivyo, tukio hilo lilivutia hisia za watu wengi duniani, baada ya Caisedo kugongwa na gari la majeruhi la timu yake mwenyewe, jambo lililomfanya aanguke na kujikunja kwa maumivu.
QUITO, ECUADOR: MASHABIKI wa soka wameachwa wakiwa na mshangao baada ya mchezaji wa El Nacional, Edison Caisedo kugongwa na kigari cha kubebea wachezaji majeruhi uwanjani cha timu yake wakati wa mechi ya Ligi Daraja la Pili Ecuador maarufu LigaPro Serie B.
El Nacional na Liga de Portoviejo zilikuwa zikimenyana katika mchezo wa ligi hiyo, ambapo wageni (Portoviejo) walishinda kwa bao 1-0. Hata hivyo, tukio hilo lilivutia hisia za watu wengi duniani, baada ya Caisedo kugongwa na gari la majeruhi la timu yake mwenyewe, jambo lililomfanya aanguke na kujikunja kwa maumivu.
Awali, katika dakika ya 71 ya mchezo mchezaji mmoja wa Portoviejo alikuwa akipatiwa matibabu akiwa amelala juu ya gari hilo akiondolewa uwanjani, lakini ghafla Caisedo alionekana akisogea lilipokuwa likipita gari hilo na kugongwa.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ecuador alianguka na kuanza kushika mguu wake kwa maumivu, huku baadhi ya makocha na viongozi wa benchi la ufundi wa timu yake wakikimbia kukabiliana na dereva wa gari hilo. Cha kushangaza zaidi ni kwamba Caisedo aliendelea kucheza hadi mwisho wa mechi licha ya tukio hilo. Hata hivyo, hakufanikiwa kusaidia timu yake kufuta pengo la bao 1-0 na kuepuka kipigo.
Mashabiki wengi kwenye mitandao ya kijamii hawakuonyesha huruma kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 36 kama ilivyokuwa kwa wachezaji wenzake, ambapo mmoja aliandika: "Ni kosa la mchezaji mwenyewe. Alijiingiza kwenye njia ya gari; ilikuwa wazi kabisa."
Mwingine amesema: "Jamaa alienda moja kwa moja mbele ya gari bila hata kuangalia." Na wa tatu aliongeza: "Hahaha, lakini kweli ni kosa la mchezaji kutembea ovyo bila kuzingatia mazingira yake."
Caisedo mwenye umri wa miaka 36, amekuwa na maisha marefu ya soka nchini Ecuador, na aliwahi kujiunga na Liga de Portoviejo akitokea El Nacional. Pia amewahi kuzichezea timu za Aucas na Orense nchini humo.