Kisa Arsenal, Ferguson aitumia meseji PSG
Muktasari:
- Arsenal ilipoteza kwa mikwaju ya penalti 4-3 kwenye mchezo mkali wa fainali uliopigwa juzi Budapest nchini Hungary baada ya dakika tisini kumalizika kwa sare ya bao 1-0 huku Arsenal ikianza kufunga na PSG kusawazisha kipindi cha pili kwa mkwaju wa penalti.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, amewatumia ujumbe mabosi wa PSG akiwaambia kuwa timu yao ilistahili kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Arsenal.
Arsenal ilipoteza kwa mikwaju ya penalti 4-3 kwenye mchezo mkali wa fainali uliopigwa juzi Budapest nchini Hungary baada ya dakika tisini kumalizika kwa sare ya bao 1-0 huku Arsenal ikianza kufunga na PSG kusawazisha kipindi cha pili kwa mkwaju wa penalti.
Staa wa Arsenal Gabriel akipoteza penati muhimu kwenye mchezo huo na kuwafanya Arsenal kushindwa kutwaa kombe la pili msimu huu baada ya awali kutwaa Ligi Kuu England baada ya kupita miaka 22. Arsenal walikuwa na umiliki wa mpira wa asilimia 24.7% tu, kiwango cha chini kabisa katika fainali ya Ligi ya Mabingwa tangu kuanzishwa jambo ambalo limewafanya wachambuzi na mashabiki wa soka kulalamika.
Kwa mujibu wa gazeti la L’Equipe, Ferguson aliandika waraka kwa rais wa PSG, Nasser Al-Khelaifi, akibainisha kuwa Arsenal walicheza mchezo wa kuzuia mno na akawaonya kwa tabia ya kucheza aina hiyo “haifurahishi”. Hata hivyo, wachambuzi kutoka Qatar Sports Investments wamesema Ferguson hakutumia neno hilo moja kwa moja, bali alisisitiza kwamba PSG walistahili kutwaa taji hilo kwa sababu walijitahidi kucheza mpira huku Arsenal wakiwa nyuma kwenye muda mwingi wa mchezo huo.
Mchezaji wa PSG, Joao Neves, pia alikosoa mtindo wa Arsenal wa kulinda zaidi ambao waliutumia Arsenal na kusema kwa mtindo huo wao walistahili kutwaa ubingwa huo: “Tumestahili taji hili. Niliona timu moja pekee ikicheza mpira, timu nyingine ilikuwa inazuia tu na kupiga mpira mbele, tulikuwa na mpira zaidi na tukicheza vyema.”