Klopp aitaka Real Madrid, Ujerumani

Muktasari:
- Kwa sasa, Klopp anafanya kazi na kampuni ya Red Bull kama Mkuu wa masuala ya Soka, baada ya kuondoka Liverpool, lakini rafiki yake wa karibu, Tanjga ambaye aliwahi kuwa mchezaji mwenzake Klopp walipokuwa Mainz amesema kocha huyo bado ana ndoto ya kufanya kazi sehemu mbili.
MADRID, HISPANIA: RAFIKI wa karibu wa Jurgen Klopp, Miroslav Tanjga amedai kocha huyo anataka kuifundisha Real Madrid na timu ya taifa ya Ujerumani kabla ya kustaafu.
Kwa sasa, Klopp anafanya kazi na kampuni ya Red Bull kama Mkuu wa masuala ya Soka, baada ya kuondoka Liverpool, lakini rafiki yake wa karibu, Tanjga ambaye aliwahi kuwa mchezaji mwenzake Klopp walipokuwa Mainz amesema kocha huyo bado ana ndoto ya kufanya kazi sehemu mbili.
Mojawapo ya kazi hizo ni ya kuifundisha Real Madrid, ambayo huenda ikawa wazi hivi karibuni, kwani Carlo Ancelotti anatarajiwa kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya Brazil.
Kazi nyingine ni ya kuinoa timu ya taifa ya Ujerumani, lakini suala la Madrid linaonekana linaweza kutimia kwa kiasi kikubwa zaidi.
Akizungumza na tovuti ya AS, Tanjga alisema:"Alichoniambia Klopp alipoondoka Liverpool ni ana matamanio mawili: kuwa kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani na wa Real Madrid. Sijui kama mojawapo itatimia. Bila shaka ni mmoja wa makocha wanaopewa nafasi ya kutua Real Madrid, lakini kwa sasa, haya yote ni uvumi mtupu. Pia najua hajawahi kujiona kama kocha wa klabu nyingine yoyote England isipokuwa Liverpool. Hataki kwenda Serie A au Ufaransa."
Klopp anatarajiwa kufuatilia kwa karibu mechi ya Leipzig dhidi ya Bayern Munich kwenye Bundesliga wikendi hii ambayo ikiwa Bayern watashinda, wataibuka mabingwa wa Bundesliga, lakini itaikosa huduma ya Harry Kane, ambaye amesimamishwa.