Man City yapewa mserereko Kombe la FA

Muktasari:
- Michuano hiyo imefikia matarajio yake kwenye raundi iliyopita baada ya mashabiki kushuhudia matokeo ya kushtua kama ilivyo kawaida ya mikikimikiki hiyo.
LONDON, ENGLAND: DROO ya raundi ya tano ya Kombe la FA imepangwa na mashabiki hawajafurahia kabisa.
Michuano hiyo imefikia matarajio yake kwenye raundi iliyopita baada ya mashabiki kushuhudia matokeo ya kushtua kama ilivyo kawaida ya mikikimikiki hiyo.
Chelsea na Tottenham zilitupwa nje ya kombe hilo zikiondolewa na wababe wenzao wa Ligi Kuu England, Brighton na Aston Villa mtawalia.
Plymouth Argyle ilishtua wengi kwenye matokeo ya raundi hiyo baada ya kuisukuma nje mabingwa mara nane, Liverpool kwenye mchezo uliofanyika Home Park, Jumapili. Droo hiyo ya raundi ya tano ilipangwa kabla ya mechi ya raundi ya nne kati ya Crystal Palace na Doncaster Rovers iliyopigwa jana Jumatatu usiku.

Mabingwa watetezi, Manchester United wamepewa mechi inayohitaji ujanja mwingi kushinda itakapoikaribisha Fulham uwanjani Old Trafford.
Plymouth, baada ya kuiduwaza Liverpool, wamejikuta kwenye bahati mbaya wakipangwa kukipiga na Manchester City uwanjani Etihad.
Jambo hilo liliwachukiza mashabiki na kuvamia mitandao ya kijamii wakidai, droo hiyo "imepangwa".
Shabiki wa kwanza alisema: "Hii droo ya Kombe la FA imepangwa. Man City imepewa mechi nyepesi nyumbani."
Shabiki wa pili aliandika: "City imepewa Plymouth? Kombe la FA limepangwa."
Shabiki wa tatu alisema: "Man City imebebwa."
Na shabiki wa nne alisema: "Man City nyumbani dhidi ya Plymouth, hii ni droo ya kupanga."

Mechi nyingine za mvuto kwenye raundi ya tano itajumuisha kipute cha Lancashire derby kati ya Preston North End na Burnley. Brighton baada ya kuitupa nje Chelsea, mechi inayofuata ni ngumu kwelikweli kwao, watakapokipiga na Newcastle United. Droo hiyo ilipangwa kabla ya mchezo wa usiku wa jana Jumanne, baina ya Exeter City na Nottingham Forest.

RATIBA KAMILI RAUNDI YA TANO KOMBE LA FA
Preston vs Burnley
Aston Villa vs Cardiff City
Crystal Palace vs Millwall
Man United vs Fulham
Newcastle vs Brighton
Bournemouth vs Wolves
Man City vs Plymouth
Exeter City/Nottm Forest vs Ipswich Town