Mastaa wa soka waliokutwa na matukio ya kutisha uwanjani

LONDON, ENGLAND. SUPASTAA, straika Sergio Aguero ameripotiwa kwamba atalazimika kufanyiwa uchunguzi wa kina wa kuhusu moyo wake ili ifahamike kwanini alipatwa na maumivu makali ya kifua akiwa uwanjani wakati wa mchezo wa La Liga timu yake ya Barcelona ilipokipiga na Alaves Jumamosi iliyopita.
Muargentina huyo alilazimika kutolewa uwanjani katika dakika ya 42 baada ya kuonekana kushindwa kupumua vizuri. Aguero inaamika kwamba aliondoka Camp Nou kwa gari la wagonjwa, kisha baadaye timu yake ya Barcelona ilifichua kwamba mchezaji wao atafanyiwa vipimo kadhaa vya afya yake kujua nini tatizo.
Kwa mujibu wa Marca, Aguero atakuwa chini ya uangalizi wa karibu kwa siku chache zijazo ili kufahamu ukubwa wa tatizo. Atafanyiwa vipimo vya moyo na kwamba hataruhusiwa kucheza hadi hapo madaktari watakapotoa ruhusa ya kitaalamu.
Aguero alikosa mechi za mwanzo wa msimu huu wa 2021-22 kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya kiazi cha mguu, lakini alicheza mechi tano zilizopita na kufunga bao moja dhidi ya Real Madrid kwenye El Clasico.
Hata hivyo, Aguero si mchezaji pekee aliyewahi kupatwa na matatizo ya kiafya akiwa uwanjani na kuzua taharuki.
Christian Eriksen
Eriksen alipata majanga hayo katika dakika 43 tu ya mechi ya ufunguzi wa michuano ya Euro iliyomalizika Julai mwaka huu, wakati Denmark ilipokuwa ikimenyana na Finland.
Kiungo huyo anayekipiga Inter Milan alipata mshtuko wa moyo uliosababisha kukosa pumzi na kupoteza fahamu, hali iliyoleta taharuki kwa wachezaji wenzake. Eriksen alipewa huduma ya kwanza na jopo la madaktari akiwa uwanjani, hali yake ikionekana kuwa mbaya na kuwahishwa hospitalini. Hata hivyo, mchezo huo uliendelea baada ya kusimama kwa muda, Denmark ikichapwa bao 1-0. Kwa sasa kiungo huyo bado hajarejea uwanjani tangu tukio hilo lilipomtokea.
Fernandos Torres
Torres alilazimika kuwahishwa hospitalini baada ya kuanguka vibaya chini akiwa uwanjani, tukio hilo limetokea Atletico Madrid ilipokuwa ikimenyana na Deportivo mwaka 2017, kipindi hicho anakipiga huko.
Straika huyo wa zamani wa Liverpool alipoteza fahamu kwenye mchezo huo, ambao Atletico ilitoka sare ya bao 1-1 kwenye mechi ya La Liga, lakini taarifa njema kutoka hospitalini ziliripoti Torres alizinduka baada ya hapo na aliendelea vizuri.
Torres amestaafu kucheza soka mwaka 2019 lakini ameonekana mara kadhaa kwenye televisheni za soka Hispania kama mchambuzi.
Iker Cassilas
Kipa wa zamani Real Madrid aliyeanza kuitumikia miamba hiyo ya Hispania tangu mwaka 1990, alianguka uwanjani akiwa mazoezini kipindi anakipiga FC Porto baada ya kupata mshtuko wa moyo mwaka 2019.
Casillas, 37, aliwahishwa hospitalini kwa ajili ya matibabu zaidi. Baada ya tukio hilo kipa huyo alikaa nje ya uwanja msimu mzima bila ya kucheza, baadaye kustaafu kucheza soka.
Fabrice Muamba
Kiungo huyo wa Bolton Wanderers alianguka uwanjani wakati wa mechi ya Kombe la FA timu hiyo ilipokuwa ikimenyana na Tottenham mwaka 2012, baada ya kupoteza fahamu kwa muda dakika 78. Daktari mmoja alibainisha kuwa Muamba ‘alikufa’ kwa muda mfupi kabla ya kuibuka upya.
Muamba alipatiwa matibabu kabla ya kuwahishwa hospitalini, akiwa uwanjani lakini baadaye alistaafu soka akiwa na umri wa miaka 24 tu.
Bafetimbi Gomis
Straika huyu wa kimataifa wa Ufaransa alianguka uwanjani mara kwa mara, imeelezwa Gomis alikuwa na matatizo ya kiafya yaliyomsababishia kuanguka kila mara uwanjani kwenye mechi kipindi anakipiga Swansea City, Galatasaray na Al-Hilal.
Marc-Vivien Foe
Kiungo huyu wa kimataifa wa Cameroon alianguka uwanjani kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho mwaka 2003, timu hiyo ilipokuwa ikimenyana na Amerika ya Kusini, madaktari walipambana kuokoa maisha yake akiwa uwanjani kabla ya kuwahishwa hospitalini, hata hivyo alifariki dunia baada ya moyo wake kusimama.
Antonio Puerta
Kiungo wa Sevilla alianguka uwanjani kwenye mechi ya La Liga timu hiyo ilipokuwa ikimenyana na Getafe msimu wa 2007 hadi 2008. Hata hivyo, Puerta aliamka baadaye akitembea kwa msaada wa madaktari na kuanguka tena kwa mara nyingine.
Nyota huyo wa kimataifa wa Hispania alipelekwa hospitalini kwa ajili ya matibabu zaidi na kufariki dunia akiwa na umri wa miaka 22.
Cheick Tiote
Miezi minne baada ya kuondoka Newcastle mwaka 2017, kiungo huyo alianguka uwanjani wakati wa mazoezi akiwa na timu ya Beijing Enterprises China. Alifariki hospitalini akiwa na umri wa miaka 30 baada ya jitihada za madaktari kuokoa maisha yake kushindikana.
Miklos Feher
Feher alipata mshituko wa moyo akiwa uwanjani wakati Benfica ilipokuwa ikimenyana na Vitoria Guimaraes, mwaka 2004. Madaktari walijaribu kuokoa maisha ya straika huyo lakini alifariki baadaye hospitali akiwa na umri wa miaka 24.