Mbio za ubingwa kwa Arsenal, Liverpool zitamalizwa hapa

Muktasari:
- Arsenal iliandikisha ushindi wake wa 12 msimu huu baada ya kuichapa Tottenham Hotspur 2-1 kwenye mchezo wa Ligi Kuu England, Jumatano iliyopita.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL imeonyesha sasa ipo siriazi kwenye mbio za ubingwa baada ya kusogea kileleni na kubakiza pointi nne tu kuifikia Liverpool kwenye msimamo.
Arsenal iliandikisha ushindi wake wa 12 msimu huu baada ya kuichapa Tottenham Hotspur 2-1 kwenye mchezo wa Ligi Kuu England, Jumatano iliyopita.
Na sasa kwa maana hiyo, mbio za kukamatia kilele cha msimamo wa ligi hazitapata mwelekeo sahihi hadi hapo Arsenal itakapomenyana na Liverpool, Mei 10.
Liverpool ya kocha Arne Slot ni kama imepungua kasi na kuonyesha kwamba chochote kinaweza kutokea kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England, ambapo miamba hiyo ya Anfield imetoka sare nne katika mechi sita zilizopita.
Hivyo, kuna sababu za kutosha kwa mashabiki wa Arsenal kufikiria kwamba kuna kitu kinaweza kufanyika kwa timu yao msimu huu, baada ya kumaliza nafasi ya pili, nyuma ya Manchester City kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England kwa misimu miwili iliyopita.
Msimu huu wa 2024-25 ni muhimu kwelikweli kwa Arsenal na kocha Mikel Arteta kumaliza ukame wa taji la Ligi Kuu England.
Arsenal na Liverpool zitachuana zenyewe kwa zenyewe Mei 10 katika mechi inayotazamiwa kuwa na upinzani mkali endapo timu zitaendelea kwa viwango vyao.
Hata hivyo, ubora wa wapinzani wao watakaochuana nao katika mechi zilizobaki kabla ya kufikia kipute chao unaweza pia kutoa taswira itakavyokuwa.
Kabla ya mchezo huo wa Anfield, Arsenal itakuwa na mechi za nyumbani dhidi ya Crystal Palace na Bournemouth. Watakuwa na mechi nyingine yenye kuhitaji ujanja na akili nyingi kuishinda ni wakati itakapokwaana na Newcastle United.
Arsenal itamalizia msimu wake kwa mechi ya ugenini dhidi ya Southampton, inatazamiwa kuwa mechi ya ushindi kwa chama la Arteta.
Kwa upande wa Liverpool, mechi mbili zao za mwisho, moja ya ugenini dhidi ya Brighton na ya nyumbani dhidi ya Crystal Palace.
Lakini, kabla ya kuwakabili Arsenal, Liverpool itakuwa Anfield kukipiga na Tottenham. Kisha itakwenda Stamford Bridge kukabiliana na Chelsea.
Na ratiba ya mechi ngumu zinazowakabili zinaweza kuwa shida kwao kutokana na kuwa na wachezaji kadhaa ambao umri wao ni mkubwa.
VITA ILIANZIA HAPA
Timu hizo mbili, Liverpool na Arsenal vita yao ya ubingwa inaanzia kwenye mechi dhidi ya wapinzani wanane ambao kila mmoja alikabiliana nao msimu huu.
Lakini, kama itahitajika kutengeneza msimamo kwenye mechi hizo, Arsenal itakuwa kileleni.
Katika mechi hizo nane, Arsenal imeshinda sita, imetoka sare moja na kupoteza moja. Kwa upande wa Liverpool, yenyewe imeshinda tano kwenye mechi hizi nane, sare mbili na kupoteza moja. Kwa upande wa mabao, Arsenal imefunga 21 katika mechi hizo na Liverpool imefunga moja zaidi, mabao 22.
Lakini, kwenye upande wa kufungwa pia, Liverpool imefungwa zaidi, mabao 11, wakati Arsenal imeruhusu mabao saba tu kwenye nyavu katika mechi hizo.
LIVERPOOL INA VITA YA MIKATABA
Liverpool imekuwa kwenye kiwango kizuri msimu huu, lakini ndani ya timu hiyo kuna kasheshe la kuhusu mikataba ya masupastaa wake, Mohamed Salah, Virgil van Dijk na Trent Alexander-Arnold, ambao wote ni wachezaji muhimu katika kikosi hicho cha Slot.
Wachezaji hao wote bado hawafahamu hatima yao kitu ambacho kinaweza kuathiri kwenye mchakato wao wa kufukuzia ubingwa. Mikataba ya wachezaji hao itafika ukomo mwisho wa msimu na hakuna yeyote aliyeonyesha kwamba anakaribia kusaini dili jipya. Van Dijk amekuwa kimya kufichua ishu ya hatima yake, wakati Alexander-Arnold anatarajiwa kwenda kujiunga na Real Madrid. Kwa upande wa Salah, alishasema, huu ni msimu wake wa mwisho Anfield.
Klabu za ng’ambo zinaweza kuwasainisha mikataba ya awali wachezaji hao watatu katika dirisha hili la Januari, kitu ambacho kitamfanya Slot kuwa kwenye wakati mgumu. Hivyo, huu ni mtihani kwao kupambana na ishu ya mikataba wakati huo ikihitaji matokeo ya uwanjani ili kutimiza malengo yao ya msimu huu ya kushinda ubingwa.
ARSENAL MAJERUHI
Arsenal ilianza msimu vizuri kabla ya kukumbana na balaa la majeruhi wengi kwenye kikosi na ni wachezaji muhimu. Arsenal ilimshuhudia nahodha wao Martin Odegaard akiwa nje muda mrefu kabla ya sasa kumpoteza mchezaji mwingine muhimu, Bukayo Saka.
Ben White, Riccardo Calafiori na Takehiro Tomiyasu nao wamekuwa majeruhi na kutibua hesabu kwenye safu ya ulinzi ya miamba hiyo inayonolewa na Mikel Arteta. Na hivi karibuni Gabriel Jesus ni mchezaji mwingine aliyeingia kwenye orodha ya wachezaji majeruhi kwenye kikosi hicho cha Emirates.
Kitu ambacho Arsenal kwa sasa inaomba kitokee ni wachezaji wake wote kurudi kwenye ubora wao. Wakiwa kwenye vita ya kushindana na Liverpool katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England itahitaji wachezaji wake kuwa fiti kwa sababu ipo pia kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Na kama wachezaji wote wa Arsenal watarudi kwenye ubora wao na kuwa fiti basi Arteta atakuwa na nguvu kubwa katika kukimbizana na Slot kwenye mbio za ubingwa.
MAN CITY KUTIBUA SHEREHE?
Taji la tano mfululizo linaweza kuwa gumu kufikiwa na Manchester City kwa msimu huu. Lakini, mabingwa hao watetezi bado kuna kitu wanaweza kukifanya kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu na kuwatibulia mipango Liverpool na Arsenal.
Chama hilo la Pep Guardiola kwa muda mrefu limekuwa na ubora mkubwa wa kuzikabili Arsenal na Liverpool kwenye mbio za ubingwa kwa miaka kadhaa. Kwa siku za hivi karibuni kikosi hicho kimeonekana kushuka ubora wake wa uwanjani. Ilifungwa na Liverpool na kutoka sare na Arsenal.
Arsenal bado ina mechi na Man City, mchezo ambao utakuwa na maana kubwa kwa Arteta na hapo ndipo linapoibuka suala la uwezekano wa Guardiola na chama lake kutibua hali ya hewa kama wenyewe watashindwa kunyakua taji hilo. Na Liverpool nayo itakuwa na mechi dhidi ya Man City uwanjani Etihad.