Mpo? Gyokeres bei yake imeshuka huko

Muktasari:
- Straika huyo ilidaiwa amefikia makubaliano ya mdomo na klabu yake itamruhusu kuondoka endapo kama kutakuwa na timu itakayokuwa imelipa ada kati ya Pauni 50.2 milioni hadi Pauni 58.5 milioni dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.
LISBON, ENGLAND: STRAIKA Victor Gyokeres amefikia makubaliano na klabu yake ya Sporting CP juu ya kuachana na timu hiyo dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi huku bei yake ikishuka chini ya Pauni 60 milioni.
Straika huyo ilidaiwa amefikia makubaliano ya mdomo na klabu yake itamruhusu kuondoka endapo kama kutakuwa na timu itakayokuwa imelipa ada kati ya Pauni 50.2 milioni hadi Pauni 58.5 milioni dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Jambo hilo limedaiwa kuzipa hamasa kubwa timu zinazohitaji huduma ya mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Sweden. Sasa timu kama Arsenal na Manchester United zitakuwa zimepata taarifa kuhusu kushuka kwa bei ya mchezaji huyo tofauti na awali ilivyokuwa ikiripotiwa kwenye mkataba wake inahitajika Pauni 83.6 milioni.
Gyokeres amekuwa kwenye rada za timu nyingi za Ulaya baada ya kiwango chake alichokionyesha huko Ureno baada ya kusajiliwa kutoka Coventry City.
Klabu hiyo ya Championship imeweka kipengele cha kupata mgawo kwenye mauzo ya mshambuliaji huyo, jambo ambalo linafanya auzwe kwa pesa nyingi.
Kinachoonekana ni fowadi huyo mwenye umri wa miaka 26 atahama dirisha lijalo na Arsenal, Liverpool na Chelsea zimeshafahamishwa kuhusu makubaliano yake na klabu ya Sporting.
Manchester City nayo inafahamu pia, ambako mkurugenzi wao mpya wa michezo, Hugo Viana, atakwenda kujiunga na miamba hiyo ya Etihad rasmi wakati wa majira ya kiangazi.
Rais wa Sporting CP, Frederico Varandas aliipuzia taarifa za Gyokoeres kuondoka, huku akishindwa kabisa kuweka bayana kuhusu hatima ya mshambuliaji huyo.
Gyokeres amefunga mabao 40 katika mechi 41 alizocheza msimu huu, wakati msimu uliopita alitupia nyavuni mara 43 katika mechi 50.