New York Knicks yaiduwaza Spurs NBA
Muktasari:
- Jalen Brunson alikuwa nyota wa mchezo huo kwa kufunga pointi 30, huku Karl-Anthony Towns akichangia pointi 18 na ribaundi 12. OG Anunoby naye aliongeza pointi 17 wakati Knicks wakifuta pengo la pointi 14 walilokuwa nyuma katika kipindi cha pili na kuibuka na ushindi muhimu ugenini.
NEW YORK, MAREKANI: New York Knicks imeanza kwa kishindo mfululizo wa fainali za NBA baada ya kuichapa San Antonio Spurs kwa pointi 105-95 katika mchezo wa kwanza wa fainali.
Jalen Brunson alikuwa nyota wa mchezo huo kwa kufunga pointi 30, huku Karl-Anthony Towns akichangia pointi 18 na ribaundi 12. OG Anunoby naye aliongeza pointi 17 wakati Knicks wakifuta pengo la pointi 14 walilokuwa nyuma katika kipindi cha pili na kuibuka na ushindi muhimu ugenini.
Ushindi huo umeifanya New York kufikisha michezo 12 mfululizo ya ushindi katika hatua za mchujo (playoffs), na kuwa timu ya saba katika historia ya NBA kufikia rekodi hiyo. Knicks pia walimaliza mchezo kwa mfululizo wa pointi 11 bila majibu na kuwa timu ya kwanza kuifunga Spurs katika Mchezo wa Kwanza wa fainali za NBA, ambapo San Antonio ilikuwa na rekodi ya ushindi 6-0.
Kwa upande wa Spurs, Victor Wembanyama alifunga pointi 26 na kukusanya ribaundi 12, ingawa alifunga mashuti sita pekee kati ya 21 aliyopiga. Stephon Castle aliongeza pointi 17, huku Julian Champagnie na Dylan Harper kila mmoja akifunga pointi 16.
Knicks waliongoza 14-7 mwanzoni mwa mchezo, lakini Spurs walijibu na kujenga uongozi wa pointi 10. Kufikia mapumziko, San Antonio walikuwa mbele kwa 55-48 na baadaye wakaongeza pengo hadi pointi 14 katika robo ya tatu. Hata hivyo, New York walijibu kwa kasi na kufunga robo hiyo kwa mfululizo wa pointi 22-9 na kufanya mchezo kuwa sare ya 76-76 kabla ya robo ya mwisho.
Dakika 2:16 kabla ya mwisho, Wembanyama alifunga mikwaju miwili ya adhabu na kuipa Spurs uongozi wa 95-94. Lakini katika shambulizi lililofuata, Brunson alipachika mpira wa alama tatu na kuirejesha Knicks mbele, uongozi ambao hawakuupoteza tena hadi mwisho wa mchezo.
Mchezo huo ulihudhuriwa na nyota na magwiji mbalimbali wa Spurs akiwemo Gregg Popovich, David Robinson, Tim Duncan na Manu Ginobili. Kwa upande wa Knicks, Patrick Ewing pamoja na mashabiki maarufu kama Spike Lee, Ben Stiller na Timothée Chalamet walikuwepo kushuhudia ushindi huo.
Mchezo wa Pili wa fainali hizo unatarajiwa kuchezwa usiku wa kuamkia kesho mjini San Antonio.