Ni vita ya Wasauzi na Wamisri CAFCL

Muktasari:
- Potezea nusu fainali za Kombe la Shirikisho Afrika zinazopigwa kesho Jumapili, leo ni Jumamosi ya kibabe wakati mechi za nusu fauinali za Ligi ya Mabingwa Afrika zitakazopigwa Afrika Kusini.
YES! Ni wikiendi ya moto. Kuanzia leo Jumamosi hadi kesho Jumapili katika michuano ya kimataifa kwa ngazi ya klabu barani Afrika.
Potezea nusu fainali za Kombe la Shirikisho Afrika zinazopigwa kesho Jumapili, leo ni Jumamosi ya kibabe wakati mechi za nusu fauinali za Ligi ya Mabingwa Afrika zitakazopigwa Afrika Kusini.
Huko kuna vita ya Wasauzi dhidi ya Wamisri na rekodi za wababe hao katika michuano hiyo sio mchezo, hali inayofanya mashabiki wasiondoke mble ya runinga zao mara filimbi itakapolia.
Al Ahly na Pyramids kutoka Misri zimesafiri kwenda Afrika ya Kusini kwa ajili ya mechi hizi ambazo zitapigwa leo kuanzia saa 10:00 jioni na kumalizwa na ile ya saa 1:00 usiku dhidi ya Mamelodi Sundowns na Orlando Pirates.

Mamelodi itaikaribisha Ahly kwenye Uwanja wa Loftus Versfeld, Pretoria ambapo katikati atasimama mwamuzi kutoka Somalia, Omar Abdulkadir Artan kbla ya Orlando kuwa wenyeji wa Pyramids katika mchezo utakaopigwa Uwanja wa Soccer City, jijini Johannesburg ambapo mwamuzi wa kati atakuwa ni Pacifique Ndabihawenimana kutoka Burundi.
Mechi hizi zinavutia watu wengi kutokana na historia na viwango ambavyo timu zote vimezionyesha tangu kuanza kwa michuano.
Ahly na Mamelodi kiujumla zimekutana mara 16, kati ya hizo tano Mamelod imeshinda na tano Ahly imeshinda huku sita zilizobakia zilimalizika kwa sare.
Katika hatua za mtoano zimewahi kukutana mara nne na katika fainali zilikutana mara moja tu mwaka 2001 , mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa Afrika Kusini ulimalizika kwa sare ya bao 1-1 kisha marudiano, Ahly ilishinda 3-1.

Katika hatua za mtoano ni Ahly ndio imekuwa na rekodi nzuri sana kwani katika misimu yote mitano iliyokutana nayo ilifanikiwa kupenya mara tatu na Mamelod mara moja.
Licha ya ubora wake wote, Al Ahly haijawahi kupata ushindi mbele ya Mamelod katika ardhi ya Afrika ya Kusini na zaidi kati ya mechi nane ilizocheza hapo iliambulia sare nne na nne ikachapika.
Mamelodi walau imewahi kupanda ushindi katika ardhi ya Misri ingawa haijawa na rekodi nzuri kwani katika mechi nane ilizocheza hapo imeshinda moja, sare mbili na tano ikachapika.
Mamelodi pia ndio inaongoza kwa kuichapa Ahly vipigo vikubwa vikubwa katika mechi ambazo imekutana nayo kwani imeshawahi kuipiga mabao matano mara mbili mwaka 2019 katika mechi ya robo fainali na mwaka 2023 katika hatua ya makundi. Mechi hizo zote zilipigwa Afrika Kusini.

Mchezaji ambaye anaongoza kwa kutupita katika mara zote ambazo timu hizi zimekutana ni Peter Shalulie mwenye mabao manne aliyofunga katika mechi sita alizocheza dhidi ya wababe hao wa Misri.
Jambo zuri kwa Mamelodi ni kuwa staa wao huyu bado yupo kikosini wakati Ahly, ambao mchezaji wao anayeongoza kwa kuwafunga Mamelodi ni Khaled Bebo na tayari alishastaafu tangu mwaka 2008.
Al Ahly ndio mabingwa wa kihistoria wa michuano hii wakiwa wameshinda mataji 12 wakati Mamelodi ikiwa na moja licha ya kufika fainali mara mbili.
Mchezo wa Orlando na Pyramids, bila shaka utatazwa sana hapa nchini na moja ya sababu mbali ya kiwango cha Wasauzi msimu huu pia itatokana na uwepo wa Fiston Mayele ambaye aliwahi kucheza hapa nchini.

Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Orlando na Pyramidskukutana tangu kuanzishwa kwao lakini Pyramid itakuwa inapambana kufuzu fainali yao ya kwanza katika historia wakati Orlando ambao ni Mabingwa wa Kombe hili mara moja watakuwa wakihitaji kufuzu fainali ya tatu.
Orlando hawajapoteza mechi zao nane zilizopita kwenye mashindano yote wakiwa wameshinda tano na tatu zikamalizika kwa sare.
Pyramids haijapata ushindi katika mechi zao tatu ilizocheza ugenini ambapo wamepoteza mara mbili mfululizo na moja ikamalizika kwa sare.
Utamu ni kwamba baadhi ya nyota wa timu hizo nne zilizotinga hatua hiyo ya nusu fainali wanachuana pia katika mbio za kuwania tuzo ya ufungaji bora wa mabao, Emam Ashour (Al Ahly) na Ibrahim Adel wa Pyramids wakiwa kileleni na mabao matano kila moja, huku Huseein El Shahat na Wessam Abou Ali (wote wa Al Ahly), Fiston Mayele (Pyramids), Peter Shalulile (Mamelodi), pamoja na Relebohile Mofokeng na Mohau Nkota (wote wa Orlando) kila moja ana mabao matatu kama waliyokuwa nao Elias Mokwana na Achref Jabri (wote wa Esperance) na Aymen Mahious (CR Belouizdad) ambao timu zao zimetolewa.
Timu hizo zitarudiana Ijumaa ijayo jijini Cairo, Al Ahly ikianza kuikaribisha Mamelodi kuanzia saa 1:00 usiku kabla ya Pyramids kumalizana na Orlando saa 3:00 usiku na zitakazokuwa zimepata matokeo mazuri ya jumla zitaenda fainali itakayopigwa kati aya Mei 26 na Juni Mosi mwaka huu.