Real Madrid yaanza kumnyatia Leao kisa Vinicius Junior

Muktasari:
- Licha ya Vinicius kuweka wazi angependa kuendelea kusalia Madrid kwa sababu anajisikia furaha kuwa hapo, mabosi wa timu hiyo wana wasiwasi anaweza kubadilisha uamuzi, hivyo wamejipanga mapema kuhakikisha wanakuwa na mbadala.
REAL Madrid inamwangalia winga wa AC Milan na timu ya taifa Ureno, Rafael Leao, 25, kama miongoni mwa mastaa ambao itawasajili dirisha lijalo la majira ya kiangazi kuziba nafasi ya Vinicius Jr kama ataamua kutimkia Saudi Arabia ambako amewekewa ofa nono.
Licha ya Vinicius kuweka wazi angependa kuendelea kusalia Madrid kwa sababu anajisikia furaha kuwa hapo, mabosi wa timu hiyo wana wasiwasi anaweza kubadilisha uamuzi, hivyo wamejipanga mapema kuhakikisha wanakuwa na mbadala.
Moja ya sababu zinazoonyesha staa huyu anaweza kuondoka ni mkataba wake ambao unamalizika mwaka 2027 na hadi sasa hajafanya makubaliano ya kuuongeza.
Leao ambaye ni miongoni mwa wachezaji tegemeo wa Milan amekuwa na uwezo mkubwa wa kufunga na kutoa asisti na msimu huu amefunga mabao 10 na asisti tisa katika mechi 43.
Moise Kean
NEWCASTLE imefanya mawasiliano ya moja kwa moja na wakala wa straika wa Fiorentina, Moise Kean, 25, ili kuipata huduma ya mkali huyu katika dirisha lijalo la uhamisho la majira ya kiangazi. Licha ya kuonyesha nia ya kumsajili, Newcastle itatakiwa kushinda vita dhidi ya Arsenal, Tottenham, AC Milan, Napoli na Barcelona. Mkataba wa sasa Kean unatarajiwa kumalizika mwaka 2029.
Joan Garcia
ARSENAL inapambana kulipa haraka Pauni 17 milioni kwa ajili ya kumsajili kipa wa Espanyol, Mhispania Joan Garcia ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028. Mabosi wa Arsenal wanataka kufanikisha dili hilo haraka baada ya kuona kuna utitiri wa timu kutoka Italia ambazo zimeanza kuiwania saini yake, hivyo inahofia kumkosa katika dakika za mwisho.
Merlin Rohl
MABOSI wa Everton wanafanya mazungumzo na wawakilishi wa Freiburg wakijadili kuhusu kiungo wa timu hiyo, Merlin Rohl, 22, ambaye ni raia wa Ujerumani.
Rohl ameonyesha kiwango bora tangu msimu uliopita na mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwakani. Msimu huu amecheza mechi 17 za michuano yote.
Eberechi Eze
ARSENAL na Liverpool ni miongoni mwa timu ambazo zipo katika vita kali ya kuiwania saini ya kiungo wa Crystal Palace na England, Eberechi Eze, 26, katika dirisha hili la usajili. Eze alikuwa mmoja kati ya mastaa waliozivutia timu nyingi kutokana na kiwango bora alichoonyesha akiwa na Palace na timu ya taifa ya England mwaka jana.
Aaron Ramsdale
KOCHA wa Newcastle, Eddie Howe ni shabiki mkubwa wa kipa wa Southampton, Aaron Ramsdale, 26, ambaye katika mkataba wake kuna kipengele kinachomruhusu kuondoka kama timu inayomhitaji italipa Pauni 25 milioni. Newcastle imeonyesha nia ya kutaka kumsajili katika dirisha lijalo. Mkataba wa staa huyu unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Milos Kerkez
BOURNEMOUTH inahitaji kiasi kisichopungua Pauni 40 milionj kwa ajili ya kumuuza beki wao wa kushoto raia wa Hungury, Milos Kerkez, 21, katika dirisha lijalo la usajili la majira ya kiangazi. Staa huyu yupo katika rada za Liverpool ambayo ipo katika mazungumzo na wawakilishi wake kuhakikisha inamsajili katika dirisha hili.
Luka Modric
KIUNGO wa Real Madrid na timu ya taifa ya Croatia, Luka Modric, 39, bado hajapokea ofa ya mkataba mpya wa kuendelea kusalia katika timu hiyo na kuna uwezekano mkubwa akatimkia Qatar ikiwa Madrid haimbakisha. Luka mkataba wake unaisha Juni mwaka huu na tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 47, nyingi akianzia benchini.