Rekodi mbaya zaiandama Man United

Muktasari:
- Mara ya mwisho kupoteza idadi hiyo ya mechi ilikuwa 989-90 ikiwa chini ya Sir Alex Ferguson na ilimaliza nafasi ya 13 katika msimamo wa Ligi Kuu England.
MANCHESTER, ENGLAND: BAADA ya kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Wolves wikiendi iliyopita, Manchester United imeendelea kuweka rekodi mbaya msimu huu ikiwa ni mara ya kwanza kupoteza mechi 15 katika msimu mmoja baada ya miaka zaidi ya 34.
Mara ya mwisho kupoteza idadi hiyo ya mechi ilikuwa 989-90 ikiwa chini ya Sir Alex Ferguson na ilimaliza nafasi ya 13 katika msimamo wa Ligi Kuu England.
Mashabiki wengi walikuwa wanataka kocha huyo afukuzwe, lakini mabosi walimvumilia na msimu ulimalizika wakishinda Kombe la FA baada ya kuichapa Crystal Palace mchezo wa fainali.

Kocha wa sasa, Ruben Amorim anatumaniwa kufuata nyayo hizo msimu huu kwa kutwaa Europa League. Ingawa hakuna dalili kuwa Amorim yupo chini ya shinikizo, ushindi wa usiku wa Alhamisi dhidi ya Lyon ulionekana kama ni kichaka cha kujifichia na kupunguza malalamiko kutoka kwa mashabiki. Man United walikuwa nyuma kwa mabao 4-2 katika muda wa ziada dhidi ya Lyon waliobaki na wachezaji 10 huko Old Trafford.
Penalti ya Bruno Fernandes dakika ya 114 iliwapa matumaini kabla ya Kobbie Mainoo kusawazisha kwa bao la kuvutia dakika ya 120 na baadaye Harry Maguire akafunga bao la ushindi.

Manchester United sasa watakutana na Athletic Bilbao na wakivuka huenda wakavaana na Tottenham Hotspur au Bodo/Glimt ya Norway katika fainali.
“Napenda kuwaambia mashabiki ukweli kwamba timu yetu bado inakosa vitu vingi. Tunapoteza nafasi nyingi. Kama hatufungi mabao, hatuwezi kushinda mechi. Tunapaswa kufanya kazi kubwa kuboresha timu hatua kwa hatua,” alisema Amorim wakati akizungumzia kikosi chake.