Roy Keane: Bruno Fernandes anaongea sana

Muktasari:
- Man United ambayo inashikilia nafasi ya 14 katika msimamo wa ligi, tangu kuanza kwa msimu huu imekuwa katika hali mbaya ikipoteza mechi 14 kati ya 32 ilizocheza.
MANCHESTER, ENGLAND: LEJENDI wa Manchester United, Roy Keane amemkosoa vikali kapteni wa timu hiyo, Bruno Fernandes kutokana na mahojiano aliyofanya baada ya timu hiyo kuchapwa mabao 4-1.
Man United ambayo inashikilia nafasi ya 14 katika msimamo wa ligi, tangu kuanza kwa msimu huu imekuwa katika hali mbaya ikipoteza mechi 14 kati ya 32 ilizocheza.
Baada ya kupoteza mechi hiyo, Man United imegeuzia silaha zake kwenye mchezo wa Europa League utakaopigwa Alhamisi ya wiki hii dhidi ya Olympique Lyon ambao mchezo wa mkondo wa kwanza walitoka nao sare baada ya Andre Onana kufanya kosa lililozaa bao la kusawazisha kwa Lyon katika dakika za mwisho.
Baada ya mechi dhidi ya Newcastle, Fernandes alisisitiza Man United inaweza kufanya vyema zaidi na akaahidi kurekebisha makosa yao kwenye mchezo ujao.
“Wachezaji wenzangu najua jinsi walivyo bora. Najua ni kazi ngumu kiasi gani kuwakilisha klabu hii. Wanataka sana kutoa kitu kwa ajili ya timu, wanataka kushinda kwa sababu wanajua jinsi watakavyokumbukwa wakishinda taji na timu hii. Alhamisi tutasonga mbele, tunapaswa kutengeneza mazingira ya kufanya hivyo, tunapaswa kuwa wa kwanza kushambulia na kutoa kila kitu tulicho nacho kwa sababu tunataka kufika nusu fainali.”
“Kwenye nyakati ngumu tumekuwa tukicheza mechi nzuri dhidi ya timu kubwa, kwenye mechi muhimu ambazo kila mtu huwa anatutazama, huwa tunasimama kwa sababu sisi ni Man United na lazima tusimame imara na tufane kila kitu ili kushinda.”
Lakini haya hayakumfurahisha Keane, ambaye alimsema Fernandes kwa kutoa kauli laini ya kupendezesha wakati timu ikiwa imetoka kuchapika vibaya.
“Bruno huwa anajitokeza mbele kila siku, lakini sasa ni kama anakuja kuongea maneno matupu tu. Hakuna maana yoyote ndani yake. Sijui kama tunaweza kusikiliza tena mahojiano ya wachezaji wa Man United kwa sababu sidhani kama wanaongea ukweli, anaendelea kuzungumzia kuwa na imani na wachezaji wenzake, lakini wac hezaji wakweli huweka matarajio kwa wenzao. Hawa si wachezaji wa timu, ni wababaishaji,” alisema Keane kujibu mahojiano ya Bruno.