Salah kumpeleka Osimhen Saudi Arabia

Muktasari:
- Osimhen ambaye hivi karibuni alidaiwa kufikia makubaliano binafsi ya kujiunga na Man United mwisho wa msimu huu, ameonekana kama mbadala wa Salah na matajiri hao wapo tayari kumpa ofa nono ambayo walipanga kumpa Mmisri huyo.
RIYADH, SAUDI ARABIA: BAADA ya kufeli katika harakati zao za kutaka kumsajili mshambuliaji wa Liverpool, Mohamed Salah dirisha lijalo la majira ya kiangazi, matajiri wa Saudi Arabia, Al-Hilal wanaripotiwa kubadilisha uelekeo na kutaka kutumia pesa hizo kwa mshambuliaji wa Napoli anayecheza kwa mkopo Galatasaray, Victor Osimhen.
Osimhen ambaye hivi karibuni alidaiwa kufikia makubaliano binafsi ya kujiunga na Man United mwisho wa msimu huu, ameonekana kama mbadala wa Salah na matajiri hao wapo tayari kumpa ofa nono ambayo walipanga kumpa Mmisri huyo.
Hali hii inarudisha mambo nyuma kwa Man United ambayo ilishaonekana kuwa katika hatua nzuri ya kumsajili Osimhen ili kuboresha eneo lao la ushambuliaji.
Kwa mujibu wa mwandishi wa habari Ben Jacobs, Al-Hilal wamehifadhi bajeti kuu waliyoitenga kwa ajili ya kumsajili Salah ambaye hivi karibuni alisaini mkataba mpya wa miaka miwili katika klabu ya Anfield. Jacobs anaongeza fedha hizo sasa zitahamishiwa kwa Osimhen, lengo likiwa ni kujenga kikosi ili kwenda kufanya vizuri kwenye Kombe la Dunia la Klabu mwaka huu.
Osimhen mwenye umri wa miaka 26, pia amekuwa akihusishwa na timu nyingine kama Chelsea na Arsenal.
Al-Hilal wanahitaji sana kusajili mshambuliaji mpya, kwa sababu kuna uwezekano straika wao Aleksandar Mitrovic, akaondoka mwisho wa msimu huu.
Hadi kufikia sasa, hatma ya dili lolote kati ya haya ipo mikononi mwa Osimhen ambaye bado hajafanya uamuzi ingawa taarifa za awali zinadai anataka kuendelea kucheza soka la kiushindani na amevutiwa na mpango wa kutua Man United.