Slot akanusha mastaa wake kuvimba

Muktasari:
- Liverpool ambayo ilipokea kichapo cha mabao 3-2 kutoka kwa Fulham ya Marco Silva wikiendi iliyopita, ilikuwa na matumaini ya kuzidi kuongeza pengo la alama kati yao na wapinzani wao Arsenal ambayo walikuwa wametoa sare ya 0-0 dhidi ya Everton.
LIVERPOOL, ENGLAND: KOCHA wa Liverpool, Arne Slot amesisitiza kwamba wachezaji wake hawajioni kama wameshachukua ubingwa na kujivuna licha ya matokeo mabaya wanayopata hivi karibuni.
Liverpool ambayo ilipokea kichapo cha mabao 3-2 kutoka kwa Fulham ya Marco Silva wikiendi iliyopita, ilikuwa na matumaini ya kuzidi kuongeza pengo la alama kati yao na wapinzani wao Arsenal ambayo walikuwa wametoa sare ya 0-0 dhidi ya Everton.
Maswali mengi yaliibuka baada ya wao kupoteza mchezo huo huku baadhi ya wachambuzi na mashabiki wakieleza kuwa huenda wachezaji wameanza kuridhika na kuona kwamba pengo la alama 11 kati ya Arsenal haliwezi kufikiwa.
Hata hivyo, Slot amesisitiza kuwa kupoteza huko kunatokana na ubora wa ligi na ushindani wanaoupokea katika kila mechi na akaipa hongera Manchester City, ambayo ilifanikiwa kuchukua mataji manne mfululizo.
Akizungumza na vyombo vya habari, Slot alisema: “Majivuno ni jambo la mwisho. Hakuna sababu ya sisi kujivunia kwa sababu hatushindi kila mechi kwa mabao matatu au manne.
“Inahitaji juhudi nyingi na kazi ngumu pamoja na ubora kushinda mechi, lakini hata timu (Manchester City) iliyoshinda ligi katika misimu minne iliyopita ilikuwa tayari imeshawahi kukutana nahali kama hii, hatuna hayo majivuno wala hali ya kuridhika, tunafahamu kikamilifu kuwa tunapaswa kushindana mechi saba zaidi. Jumatano (dhidi ya Everton) ilikuwa mechi ngumu na hii pia ilikuwa ngumu, lakini mara nyingi tumekuwa upande wa kushinda, lakini leo tumekosa.”
Liverpool itarejea uwanjani mwishoni mwa wiki hii kuvaana na West Ham katika dimba la Anfield.