UBINGWA EPL: Liverpool inaisikilizia Arsenal

Muktasari:
- Liverpool kwa sasa haina presha na ubingwa na kila mtu anajua ubingwa ni Majogoo hao wa Anfield na ni suala la muda tu kutangazwa rasmi.
LONDON, ENGLAND: WIKI hii wachezaji na mashabiki wa Liverpool watakuwa sebuleni macho yote yakiutazama mchezo wa London dabi wa Arsenal dhidi ya Crystal Palace wa keshokutwa Jumatano, utakaoamua ubingwa wao wa Ligi Kuu England msimu huu.
Liverpool kwa sasa haina presha na ubingwa na kila mtu anajua ubingwa ni Majogoo hao wa Anfield na ni suala la muda tu kutangazwa rasmi.
Hata hivyo, wakiwa wanasubiria mchezo wao ujao wa ligi dhidi ya Tottenham wikiendi ijayo, Aprili 27, wachezaji na mashabiki wa Liverpool wanaweza kwenda katika mchezo huo wakiwa na furaha ya ubingwa na wanachoombea ni Washika mitutu hao wapoteze kwa Palace.
Baada ya ushindi wa wikiendi iliyopita wa bao 1-0 dhidi ya Leicester ugenini, Liverpool ilikuwa inasubiri Arsenal ipoteze mbele ya Ipswich Town na kutangaza ubingwa kabla ya Arsenal kushinda mabao 4-0 na kuisubirisha tena.
Endapo Arsenal itashinda mchezo huo, hatma ya ubingwa kwa Liverpool itabaki kwao wenyewe na itatakiwa kushinda dhidi ya wapinzani wagumu Tottenham Jumapili ijayo.
Kwa sasa Arsenal iliyopo nafasi ya pili ina pointi 66 wakati vinara Liverpool ina 79 na timu zote zimeshacheza mechi 33.
Ikiwa Arsenal itashinda mechi zake tano zote zilizosalia itafikisha pointi 81 wakati Liverpool ikishinda mechi moja tu itakuwa na pointi 82.
Pia, Arsenal itakapopoteza mechi yao moja itakuwa na maana hata ikishinda minne itakayosalia itafikisha pointi 78 tu ambazo tayari Liverpool imeshazivuka.
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amesisitiza yeye na wachezaji wake watapambana kuhakikisha wanashinda kila mechi ili Liverpool isije kutangaza ubingwa kwa wao kupoteza mchezo.
Akizungumza kabla ya mchezo wao dhidi ya Ipswich uliomalizika kwa kushinda mabao 4-0, Arteta alisema:
“Tutaakikisha tunashinda mechi dhidi ya Ipswich, ili hilo suala la Liverpool kushinda ligi kupitia sisi lisitokee.”
Matokeo ya Arsenal yanaonekana kufaidisha timu nyingi kwani wikiendi baada ya ushindi wao dhidi ya Ipswich, Man United pia ilifaidika nayo kwa kujihakikishia kuendelea kusalia Ligi Kuu England msimu ujao kwani hata ikipoteza mechi zote zilizosalia bado haitoweza kufikiwa na Ipswich iliyopo nafasi ya 18 ikiwa na pointi 21.