Ubingwa NBA... ‘Nova Knicks wanavyoweza kuweka historia dhidi ya Spurs
Muktasari:
- Kundi adimu ambalo Brunson, Bridges na Hart wanaweza kuungana nalo kwa kushinda fainali za NBA zilizoanza kuchezwa wiki hii na leo asubuhi ikitarajiwa ya pili ni lile la mastaa waliopita ambao walikiwasha na kuvuta ndoo ya ubingwa, na iwapo wataiongoza Knicks kutwaa, wataungana na jozi nne za wachezaji wenza katika historia ya mpira wa kikapu ambao wameshinda ubingwa wa Ligi ya Kikapu Marekani Ngazi ya Vyuo maarufu kama NCAA na NBA.
NEW YORK, MAREKANI: LEO saa 9:30 usiku fainali ya pili ya Ligi ya Kikapu Marekani maarufu NBA imepigwa baada ya ile ya kwanza kumalizika kwa ushindi New York Knicks kushinda kwa pointi 105 dhidi ya 95 za Sun Antonio Spurs.
Siyo tu kwamba Knicks wana nafasi ya kutwaa ubingwa wao wa kwanza tangu 1973, bali wana wachezaji watatu kina Jalen Brunson, Mikal Bridges na Josh Hart wenye nafasi ya kuingia katika kundi adimu kwa kuongeza ubingwa wa NBA kwenye mafanikio.
Kundi adimu ambalo Brunson, Bridges na Hart wanaweza kuungana nalo kwa kushinda fainali za NBA zilizoanza kuchezwa wiki hii na leo asubuhi ikitarajiwa ya pili ni lile la mastaa waliopita ambao walikiwasha na kuvuta ndoo ya ubingwa, na iwapo wataiongoza Knicks kutwaa, wataungana na jozi nne za wachezaji wenza katika historia ya mpira wa kikapu ambao wameshinda ubingwa wa Ligi ya Kikapu Marekani Ngazi ya Vyuo maarufu kama NCAA na NBA.
Bill Russell na Sam Jones walishinda mataji mawili wakikicheza Chuo Kikuu cha San Francisco katika miaka ya 1950, kisha wakawa wachezaji wenza katika mataji manane ya NBA kama sehemu ya Boston Celtics waliotawala miaka ya 1950 na 1960. Baadaye, John Havlicek na Larry Siegfried waliungana na Russell na Jones katika vikosi vya mabingwa vilivyoongozwa na Red Auerbach, ambapo walishinda mataji matano ya NBA pamoja mjini Boston.
Hata hivyo, kabla ya hapo wawili hao waliisaidia Ohio State Buckeyes ya Fred Taylor kushinda ubingwa wa NCAA msimu wa 1959-60. Alipokuwa bado anajulikana kama Lew Alcindor, Kareem Abdul-Jabbar alijenga utamaduni wa ushindi akiwa pamoja na mwenzake wa UCLA, Lucius Allen, katika kikosi maarufu cha Bruins kilichoongozwa na John Wooden katika miaka ya 1960, wakishinda mataji mawili kabla ya wawili hao kushinda ubingwa wa NBA pamoja na Bucks.
Antoine Walker na Derek Anderson walikuwa sehemu ya kikosi mashuhuri cha Kentucky kilichofundishwa na Rick Pitino ambacho kilishinda ubingwa wa taifa kwa msaada wa wachezaji tisa waliokuja kucheza NBA baadaye. Walker na Anderson walikutana tena kama wachezaji wenza baada ya Anderson kuhamishiwa Miami Heat katikati ya msimu wa 2005-06 ambao uliishia kwa ubingwa huko South Beach.
NOVA KNICKS’ WALIVYOKUSANYIKA
Nova Knicks au mara nyingine huandikwa Villanova Knicks ni jina la utani la timu ya New York Knicks kutokana na kundi la wachezaji wake waliowahi kucheza Chuo Kikuu cha Villanova University, na sio jina rasmi la timu, bali ni ‘nickname’ ya mashabiki na vyombo vya habari kuelezea kundi hilo maalumu la wachezaji ndani ya Knicks.
Jina hilo linatumika kwa sababu Knicks walikuwa na au bado wana wachezaji waliotoka Villanova ambao walicheza pamoja na kuleta makali kikosini (chemistry) kama ilivyo kina Brunson, Hart na Bridges na wengine wakati fulani kama Donte DiVincenzo.
Brunson, Bridges na Hart walijenga msingi wa ushindi muda mrefu kabla ya kuingia Madison Square Garden kuchezea Knicks. Watatu hao waliwasili katika Chuo Kikuu cha Villanova chini ya kocha maarufu wa zamani Jay Wright katika misimu iliyofuatana; Hart aliwasili kwanza 2013, Bridges 2014 na hatimaye Brunson kama mmoja wa wachezaji bora waliokuwa wakijiunga na vyuo 2015.
Watatu hao waliungana na mchezaji mwingine wa zamani wa Knicks, Donte DiVincenzo, ambaye alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza msimu wa 2015-16. Mwaka huo, wanne hao waliisaidia Villanova Wildcats kushinda ubingwa wa kwanza wa taifa wa vyuo tangu 1984-85.
Hart alihitimu chuo akiwa amemaliza kwa mafanikio makubwa, lakini Brunson, Bridges na DiVincenzo waliendelea kubaki chuoni na misimu miwili baadaye waliisaidia Villanova kushinda ubingwa mwingine wa taifa.
Nyota hao wanne wa zamani wa Villanova waliendelea na njia zao tofauti NBA, lakini kana kwamba Knicks walikuwa dira yao, waliibukia tena pamoja baada ya miaka kadhaa. Safari hii, Brunson ndiye aliyewasili kwanza baada ya kusaini kama mchezaji huru katika majira ya joto 2022.
Msimu uliofuata, Knicks ilimpata Hart kupitia dirisha la usajili wa kubadilishana wachezaji, kisha ikamsajili DiVincenzo majira ya joto 2023.
Brunson na Hart, ambao waliwahi kuishi chumba kimoja Villanova, walitumia uzoefu huo kuanzisha podikasti, ambayo pia ilimshirikisha DiVincenzo mara kwa mara. Wakati wote huo, watatu hao waliendelea kuchangia ushindi mwingi kama walivyofanya walipokuwa Villanova Wildcats.
Brunson na Hart waliisaidia Knicks kufika nusu fainali za Ukanda wa Mashariki 2023 kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 10, kisha DiVincenzo aliisaidia klabu hiyo kufikia hatua hiyo tena 2024 huku akiwa gumzo la Jiji la New York.
Wakati Knicks ilipotoa machaguo matano ya raundi ya kwanza pamoja na Bojan Bogdanovic kwenda Brooklyn ili kumpata Bridges katika majira ya joto ya 2024, kikosi hicho cha marafiki wanne kilikutana tena rasmi. Hata hivyo, hali hiyo haikudumu kwa muda mrefu.
Miezi michache baadaye, DiVincenzo alihamishwa kwenda Timberwolves katika biashara ya timu tatu iliyomleta Karl-Anthony Towns mjini New York. Lakini Brunson, Bridges na Hart wameendelea kubaki pamoja na sasa wako hatua chache tu kutwaa ubingwa na kuandika historia katika mpira wa kikapu.
Kwa kuzingatia idadi kubwa ya wachezaji wa zamani wa Villanova waliopo katika kikosi cha Knicks, jambo hilo linafanya kujiuliza, vikosi vya Knicks na Spurs vinaonekanaje vinapogawanywa kulingana na mastaa na vyuo walivyochezea?
Hata hivyo, pia kuna uwakilishi wa vyuo vidogo katika New York Knicks, kwani mchezaji wa kati Mitchell Robinson alichezea Western Kentucky ya Conference, huku walinzi Landry Shamet na Jordan Clarkson wakicheza angalau msimu mmoja AAC. Yote katika yote ni kwamba, je ubingwa NBA utaangukia Knicks au utatua Spurs? Bado kuna mechi kadhaa mbele za kuamua.