Fainali NBA mambo yanaanza
Muktasari:
- Spurs, wakiongozwa na nyota wao kijana Victor Wembanyama, wamefuzu kucheza Fainali za NBA kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2014. Mara ya mwisho walipofika hatua hiyo waliibuka mabingwa baada ya kuichapa Miami Heat ya LeBron James na kunyakua kombe la Larry O’Brien.
NEW YORK, MAREKANI: HATIMAYE pazia la Fainali za NBA limefunguliwa leo alfajiri, huku New York Knicks na San Antonio Spurs zikikabiliana katika vita ya kuwania ubingwa unaoweza kumaliza ukame wa muda mrefu wa mataji kwa pande zote mbili.
Spurs, wakiongozwa na nyota wao kijana Victor Wembanyama, wamefuzu kucheza Fainali za NBA kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2014. Mara ya mwisho walipofika hatua hiyo waliibuka mabingwa baada ya kuichapa Miami Heat ya LeBron James na kunyakua kombe la Larry O’Brien.
Kwa upande wa Knicks, safari yao ya kurejea fainali imekuwa ndefu zaidi. Wamefika hatua hii baada ya kushinda michezo 11 mfululizo na sasa wanacheza Fainali za NBA kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1999. Cha kuvutia, mpinzani wao wakati huo alikuwa pia San Antonio Spurs.
Knicks hawajatwaa ubingwa wa NBA tangu mwaka 1973, hivyo kusubiri kwa miaka 53 sasa kunawapa hamasa kubwa ya kuandika historia mpya.
Hii ina maana kuwa NBA itapata bingwa mpya kwa msimu wa nane mfululizo, jambo linaloonyesha ushindani mkubwa unaoendelea kuongezeka kwenye ligi hiyo maarufu zaidi ya kikapu duniani ikiwa na mastaa wakubwa wanaolipwa mikwanja mirefu.
JINSI WALIVYOFIKA FAINALI
San Antonio Spurs walionyesha nguvu ya kupambana baada ya kutoka nyuma kwa michezo 3-2 na hatimaye kuwaondoa mabingwa watetezi, Oklahoma City Thunder, katika Fainali za Kanda ya Magharibi.
Kwa Knicks, mambo yalikuwa mepesi zaidi. Waliichapa Cleveland Cavaliers kwa ushindi wa 4-0 katika Fainali za Kanda ya Mashariki na kuingia fainali wakiwa katika kiwango bora kabisa (Hii maana yake walishinda michezo minne kati ya saba). Fainali za NBA huchezwa kwa mfumo wa best-of-seven na timu ya kwanza kushinda michezo minne hutawazwa bingwa.
Michezo miwili ya kwanza itafanyika katika Ukumbi wa Spurs, Frost Bank Center, kutokana na kumaliza msimu wa kawaida ikiwa na nafasi ya juu zaidi. Baada ya hapo, michezo miwili inayofuata itahamia New York katika ukumbi maarufu wa Madison Square Garden.
Endapo kutahitajika, mchezo wa tano utachezwa San Antonio, wa sita New York, huku mchezo wa saba na wa mwisho ukifanyika tena nyumbani kwa Spurs na kuwapa faida ya kuweza kutwaa ubingwa huo.