Wachezaji 5 hatari wa NBA ambao hawakuwahi kubeba ubingwa
Muktasari:
- Licha ya mafanikio yao binafsi, walikosa kile kinachochukuliwa kama mafanikio makubwa zaidi katika mpira wa kikapu.
BOSTON, MAREKANI: KATIKA historia ya NBA, kuna wachezaji wengi waliokuwa na vipaji vikubwa lakini hawakuwahi kushinda ubingwa.
Licha ya mafanikio yao binafsi, walikosa kile kinachochukuliwa kama mafanikio makubwa zaidi katika mpira wa kikapu.
Hawa ni wachezaji watano waliotamba sana katika ligi hiyo maarufu zaidi duniani, lakini walibaki bila ubingwa yaani championship ring.
Kila mmoja alikuwa balaa katika mchezo huu, lakini ndo hivyo tena imebaki kuwa historia.
KARL MALONE
Alikuwa mmoja wa wafungaji bora kabisa katika historia ya NBA. Alijulikana kwa uimara wake, nidhamu ya hali ya juu na uwezo wake wa kufunga pointi karibu kila mchezo. Jina lake la utani “The Mailman” lilimaanisha kuwa kila mara alitimiza wajibu wake wa kufunga pointi.
Katika maisha yake ya NBA, Malone alicheza muda mwingi na Utah Jazz (1997 na ‘98). Ushirikiano wake na John Stockton uliifanya Jazz kuwa moja ya timu hatari zaidi katika ligi kwa miaka mingi. Walikuwa na maelewano mazuri sana uwanjani.
Malone alishinda tuzo ya MVP mara mbili, jambo linaloonyesha kiwango chake kikubwa cha ubora. Pia aliweka rekodi nyingi za kufunga pointi na kuwa mmoja wa wafungaji bora wa muda wote katika NBA.
Licha ya mafanikio hayo yote, alikumbana na changamoto kubwa alipofika fainali. Mara mbili alikutana na Chicago Bulls iliyoongozwa na Michael Jordan na kushindwa kushinda ubingwa.
Hadi anastaafu, Malone alibaki kuwa mmoja wa wachezaji bora kabisa bila ubingwa. Hata hivyo, mchango wake katika mchezo wa mpira wa kikapu unaendelea kuheshimiwa hadi leo.
CHARLES BARKLEY
Alikuwa mchezaji mwenye nguvu, kasi na ujasiri mkubwa uwanjani. Licha ya kuwa mfupi kwa nafasi yake, alishindana na wachezaji warefu na kuwazidi uwezo.
Alijulikana kwa uwezo wake wa kufunga pointi na kuchukua ‘rebound’ kwa ustadi mkubwa. Barkley alikuwa na kipaji cha kipekee kilichomfanya awe tishio kwa timu pinzani kila alipokuwa uwanjani.
Mwaka 1993, Barkley alishinda tuzo ya MVP na kuiongoza Phoenix Suns hadi fainali za NBA. Hiki ni kipindi ambacho alikuwa katika kilele cha ubora wake.
Hata hivyo, walikutana na Chicago Bulls ya Michael Jordan na kushindwa katika fainali. Hii ilikuwa nafasi yake kubwa zaidi kushinda ubingwa, lakini haikuwezekana.
Baada ya kustaafu, Barkley alibaki kuwa mmoja wa wachezaji wanaoheshimiwa sana. Ingawa hakuwahi kushinda ubingwa, jina lake linaendelea kuwa kubwa katika historia ya NBA.
JOHN STOCKTON
Ni mmoja wa walinzi bora zaidi kuwahi kucheza NBA. Alijulikana kwa akili yake ya mchezo, uwezo wa kutoa pasi sahihi na uongozi wake uwanjani.
Stockton anashikilia rekodi ya muda wote ya pasi za mwisho (assists) na kuiba mipira (steals), jambo linaloonyesha ubora wake wa kipekee katika nafasi yake.
Katika maisha yake yote ya NBA, alicheza na Utah Jazz pekee. Ushirikiano wake na Karl Malone uliifanya timu hiyo kuwa tishio kubwa kwa timu nyingine.
Walifanikiwa kufika fainali za NBA mara mbili, lakini walishindwa na Chicago Bulls iliyoongozwa na Michael Jordan. Hii iliwanyima nafasi ya kushinda ubingwa.
JAMES HARDEN
Anatajwa kuwa mmoja wa wafungaji bora wa kizazi cha sasa cha NBA. Alijulikana kwa uwezo wake wa kufunga pointi nyingi.
Akiwa na Houston Rockets, Harden alikuwa na misimu mingi ya kuvutia sana, akiongoza ligi kwa kufunga pointi. Alishinda tuzo ya MVP mwaka 2018.
Mtindo wake wa kucheza, hasa hatua ya nyuma (step-back three), ulimfanya awe hatari sana kwa wapinzani. Pia alikuwa mzuri katika kupata faulo na kufunga kwa adhabu.
Hata hivyo, licha ya mafanikio yake binafsi, hakufanikiwa kushinda ubingwa. Mara nyingi timu zake zilikwama katika hatua za mwisho za playoff.
Harden bado anahesabika kama mmoja wa wachezaji bora lakini ukosefu wa ubingwa unaendelea kuwa sehemu ya mjadala kumhusu.
ALLEN IVERSON
Alikuwa mmoja wa wachezaji wenye mvuto mkubwa zaidi katika historia ya NBA. Alijulikana kwa jina la utani “The Answer” kutokana na uwezo wake wa kushinda michezo.
Licha ya kuwa na kimo kifupi, Iverson alikuwa na kasi, mbinu na ujasiri uliomfanya awe hatari sana kwa wapinzani. Alikuwa mmoja wa wafungaji bora wa wakati wake.
Mwaka 2001, alishinda tuzo ya MVP na kuiongoza Philadelphia 76ers hadi fainali za NBA. Huu ulikuwa wakati wake bora zaidi.
Hata hivyo, walishindwa na Los Angeles Lakers iliyokuwa na mastaa wakubwa kama Shaquille O’Neal na Kobe Bryant.