Hornets yaibuka upya NBA
Muktasari:
- Baada ya kukaa nje ya mchujo ‘playoffs’ kwa kipindi cha miaka tisa mfululizo rekodi mbaya zaidi kwao katika ukanda wa Mashariki, hivi sasa Hornets wanaonyesha dalili zote za kurejea kwenye ushindani mkubwa.
LOS ANGELES, MAREKANI: CHARLOTTE Hornets imegeuka kuwa moja ya stori kubwa na za yakusisimua katika msimu wa 2025/26 wa NBA, baada ya kuonyesha mabadiliko makubwa yaliyowashangaza wachambuzi na mashabiki wa mchezo huo.
Baada ya kukaa nje ya mchujo ‘playoffs’ kwa kipindi cha miaka tisa mfululizo rekodi mbaya zaidi kwao katika ukanda wa Mashariki, hivi sasa Hornets wanaonyesha dalili zote za kurejea kwenye ushindani mkubwa.
Mwanzoni mwa msimu, hali haikuwa nzuri kwa timu hiyo. Walikuwa na rekodi ya ushindi wa mechi 16 dhidi ya kupoteza 28 kufikia Januari, jambo lililoashiria uwezekano wa kuendeleza ukame wao wa kucheza hatua ya mtoano hadi miaka kumi.
Hata hivyo, mambo yamebadilika kwa kasi katika miezi ya hivi karibuni, ambapo wameshinda michezo 22 kati ya 28 iliyofuata matokeo yaliyowapa matumaini mapya.
NINI WAMEFANYA
Kwa mujibu wa takwimu za NBA, Hornets wamepiga hatua kubwa sana ukilinganisha na msimu uliopita. Kutoka kuwa miongoni mwa timu dhaifu zaidi kwa kuruhusu wapinzani kuwazidi kwa wastani wa pointi 9.1 kwa kila mashambulizi 100, sasa wamebadilika na kufikia wastani wa ziada ya pointi 4.7.
Hili ni ongezeko la pointi 13.8 likiwa moja ya maboresho makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 30 iliyopita. Takwimu hizi zinaweka Hornets katika kundi la timu chache sana zilizowahi kubadilika kwa kiwango kikubwa namna hii ndani ya msimu mmoja.
Mafanikio haya yametokana zaidi na kuimarika kwa safu ya ushambuliaji, ambayo sasa inafunga pointi nyingi zaidi kwa ufanisi mkubwa. Wameongeza wastani wa pointi 11.5 kwa kila mashambulizi 100 ukilinganisha na msimu uliopita ongezeko kubwa kuliko timu nyingine yoyote msimu huu.
Pia safu ya ulinzi nayo imeimarika kwa kiasi kikubwa, huku Hornets wakiruhusu pointi chache zaidi na kuonyesha uwezo mzuri katika kupambana na mipira ya kurudi (rebounds) pande zote mbili za uwanja. Kwa sasa, ni miongoni mwa timu chache zinazofanya vizuri katika kushambulia na kulinda kwa uwiano mzuri.
NYOTA CHIPUKIZI
Mabadiliko hayo hayawezi kuelezwa bila kuwataja wachezaji muhimu kama LaMelo Ball na Brandon Miller, ambao wamekuwa mhimili mkubwa wa mafanikio ya timu hiyo.
LaMelo Ball, ambaye mara nyingi alikumbwa na majeraha katika misimu iliyopita, amekuwa katika hali nzuri ya kiafya msimu huu na kucheza mechi nyingi zaidi. Hali hii imemwezesha kuwa na mchango mkubwa zaidi uwanjani.
Kwa upande wake, Brandon Miller ameendelea kukua kwa kasi na kuwa mmoja wa wachezaji wenye mchango mkubwa ndani ya kikosi. Ushirikiano wao wawili umeongeza ubora wa timu, hasa wanapokuwa pamoja uwanjani.
USHINDI WA KISHINDO
Moja ya mambo ya kipekee kwa Hornets msimu huu ni namna wanavyoshinda michezo yao. Ushindi wao mara nyingi umekuwa wa kishindo wakishinda kwa wastani wa pointi 18 kwa kila mchezo wanaoshinda rekodi ambayo haijawahi kushuhudiwa mara nyingi katika historia ya NBA.
Hata hivyo, upande wa pili wa sarafu unaonyesha changamoto. Hornets wamekuwa wakipata ugumu mkubwa katika michezo iliyo na ushindani mkubwa, hasa pale ambapo matokeo yanaamuliwa katika dakika za mwisho.
Takwimu zinaonyesha kuwa wamekuwa na rekodi mbaya katika michezo yenye tofauti ndogo ya pointi katika dakika za mwisho, huku pia wakikosa ufanisi katika upigaji wa mipira ya pointi tatu wakati wa nyakati hizo muhimu.
Hii inaonyesha wazi kuwa, licha ya ubora wao wa jumla, bado wanahitaji uzoefu na utulivu katika kumaliza michezo mikubwa.
RATIBA NGUMU
Licha ya mafanikio yote hayo, safari ya mchujo ‘playoffs’ bado sio rahisi kwa Hornets. Ratiba yao iliyobaki ni ngumui, kwani wanakutana na timu nyingi zenye rekodi nzuri na ushindani mkubwa.
Hii ina maana kuwa kila mchezo uliosalia ni muhimu, na utahitaji kiwango cha juu cha nidhamu, umakini na ubora ili kuhakikisha wanapata matokeo chanya.
Kwa ujumla, Charlotte Hornets wameonyesha mabadiliko makubwa yanayoweza kuwa mwanzo wa enzi mpya kwa klabu hiyo. Wamejenga msingi imara wa kikosi chenye vipaji, nguvu na ari ya ushindani.
Iwapo wataweza kurekebisha mapungufu yao basi hakuna shaka kuwa wana uwezo wa kuvunja ukame wa miaka mingi bila ya kucheza hatua ya mchujo.